Na Mwandishi wa A24tv Arusha.
Benki ya NMB imefanikiwa kuwapa semina watumishi wa umma wanaokaribia kustaafu juu ya fursa za kiuwekezaji wanazoweza kujiongezea kipato kutokana na fedha za mafao wanayotarajia kupokea.
Akizungumza na watumishi wa umma zaidi ya 150 wanaokaribia kustaafu Mkoani Arusha, Meneja Mahusiano amana za wateja kutoka Benki ya NMB Monica Job amesema kuwa wameamua kutoa Elimu hiyo ili kuwaepusha wastaafu na matapeli.
“Leo tumekuja kuwajulisha wastaafu watarajiwa juu ya masuluhisho ya kifedha tuliyonayo kwa ajili yao kuanzia miamala ya kawaida, akaunti maalumu ya wastaafu tunayoiita ‘Wisdom akaunti’ lakini pia mikopo mbalimbali” amesema Monica.
Monica amesema, katika kuhakikisha masuluhisho hayo yanafikia walengwa wameanzisha klabu yenye zaidi ya wastaafu 70,000 ambao wanaunganishwa pamoja na kupata nafasi ya kukutana na wenzao waliotangulia kubadilishana uzoefu wa maisha nje ya ajira na kuunganishiana fursa za uwekezaji, biashara, kilimo na ufugaji.
“Katika klanu hizo, tumekuwa tukiwakutanisha mara kwa mara na wataalamu wa Afya, uwekezaji, kilimo na ufugaji na kupata elimu ya kazi zao, changamoto na fursa mpya ikiwemo mabadiliko ya sheria ili kuepuka kuingia kwenye matatizo, lengo wawe na uhakika wa kipato hata nje ya ajira binafsi”.
Akifungua semina hiyo, katibu tawala Mkoa wa Arusha Missaile Mussa amewataka watumishi hao kuzingatia elimu wanayoipata hasa matumizi ya fedha hizo na kuepukana na maelekezo ya watu wanaojifanya wanatoka taasisi za fedha wanaowapigia simu.
“Elimu hii ni muhimu sana kwani maisha mazuri yanaanzia unapostaafu na maisha mabaya pia yanaanzia hapo hapo usipokuwa na nidhamu katika matumizi ya fedha hizo za mafao na pensheni”amesema na kuongeza;
“Lakini pia epukaneni na matapeli ambao wanawapigia simu eti wanatoka taasisi za kifedha, hiyo ni changa la macho na hatutakuwa na msaada na wewe, pia kuweni makini na vijana wadogo ambao mkishapata fedha wanajidai kuwapenda” amesema Mussa.
Zaidi ya hayo aliwaonya watumishi hao kuhakikisha wanatunza siri za serikali hata wanapostaafu ili kuendelea kuliweka taifa katika hali ya usalama na utulivu.
“Kuna mengi unayoyafahamu kwenye kitengo chako, unapostaafu hakikisha inabaki siri, sio ndio umefunguliwa kwenda kuyasemasema kwani mengine unaweza kusema ukaleta taharuki au kuwanyima watu imani na serikali yao au hata kuvunja na kuhatarisha usalama wa nchi hivyo kuweni makini sana”.
Awali, Kaimu Mkurugenzi wa mfuko wa PSSSF, Mbaruku Magawa alisema lengo la semina hiyo ya kila mwaka ni kuwaandaa wanachama wanaokaribia kustaafu kutumia fedha zao za mafao vema katika uwekezaji wenye tija ili kumudu maisha mapya ya kustaafu.
Amesema kwa mwaka huu zaidi ya wastaafu 3300 wanaokaribia kustaafu wameelimishwa juu ya matumizi ya mafao yao watakayolipwa hasa yaelekezwe kwenye miradi yatakayotoa mchango na ajira kwa vijana sambamba na kuongeza pato la mstaafu na Taifa kwa ujumla.
Mwisho