Site icon A24TV News

BoT YAJIZATITI KUIMARISHA MIFUMO YA UKUSANYAJI MAPATO

Na Richard Mrusha

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, amewataka Watanzania kuendelea kutumia huduma zinazotolewa na BoT kwa kuwa benki hiyo imeimarisha mifumo yake, hususan ile inayowezesha ukusanyaji wa mapato ya serikali.

Tutuba ameyasema hayo siku ya Ijumaa Desemba 20, 2024 wakati ujumbe wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ulipofika katika ofisi za BoT kwa lengo la kuwapongeza na kutoa shukurani kwa Tutuba na watendaji wote walio chini ya taasisi anayoiongoza.

“Kila mmoja ahakikishe anatumia mifumo iliyopo, mifumo yetu iko imara, madhubuti na haina changamoto zinazoweza kukwamisha ukusanyaji wa mapato”, ameeleza Tutuba.

Amesema BoT imejipanga vizuri kuhakikisha yeyote anayetaka kulipa analipa vyema kutokana na uwepo wa mifumo imara ambayo ipo chini ya idara mbalimbali za benki hiyo zinazowezesha ulipaji wa kodi kama Idara ya Benki, Idara ya Mifumo na Idara ya Mifumo ya Malipo.

“Niwahakikishie kwamba akaunti zote za serikali zipo salama, sisi tunasimamia akaunti za serikali na akaunti za mabenki, ndilo jukumu letu la kisheria kuhakikisha zipo salama, na kupitia taasisi zetu au idara tulizonazo zinawezesha kusimamia akaunti za watu binafsi zilizoko kule kwenye mabenki”, ameeleza Tutuba.

Sambamba na kuwashukuru TRA kwa kuendelea kufanya kazi ya kusimamia kwa weledi ukusanyaji wa mapato, Tutuba amesema wao kama BoT wanatambua umuhimu wa kulipa kodi na wanatimiza wajibu wao pia kama mawakala wa kukusanya kodi. Kutokana na hilo, amewahakikishia TRA kuwa wataongeza muda wa wananchi kulipa kwenye mabenki hasa kipindi hiki cha sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Fedha kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Dinah Edward akimwakilisha Kamishna Mkuu wa TRA Yusuph Mwenda, amemshukuru Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Emmanuel Tutuba kwa ushirikiano ambao umekuwepo kati ya taasisi hizo mbili katika utendaji wao wa kila siku.

Amesema kuwa katika Mwaka wa Fedha 2024/2025, TRA imekasimiwa jukumu la kukusanya takribani Shilingi trilioni 31.05 likiwa ni lengo ghafi ambapo hadi kufikia mwezi Novemba TRA imekusanya Shilingi trilioni 12. 94 sawa na 105.1% ya lengo ambalo ilipaswa kulifikia mpaka kipindi hicho (Novemba), na asilimia 41.67 ya lengo la mwaka mzima, suala ambalo limepongezwa na Gavana Tutuba.

“Ni dhahiri kuwa ufikiwaji wa lengo hilo hadi kufikia Juni 2025 unahitaji ushirikiano na walipakodi, pamoja na wadau mbalimbali ambao wanahusika katika mnyororo mzima wa kufanikisha ukusanyaji wa mapato hayo”, ameeleza Dinah.

Aidha amesema ushiriki wa BoT umejipambamua katika maeneo ya kisera na utendaji wa moja kwa moja ikiwamo usimamiaji wa mabenki, uhamishaji wa fedha na maboresho ya mifumo.

“Yote haya yana mchango chanya katika kutanua wigo wa kodi na walipakodi, kuleta wepesi kwenye ulipaji wa kodi na kuboresha usimamizi wa mapato yanayoratibiwa na TRA, sambamba na hilo BoT kama taasisi na yenyewe ni sehemu ya walipakodi”, ameeleza.