Na Mwadishi wa A24tv .Arusha .
Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA kwa kuongeza makusanyo ya kodi kutoka sh. trilioni 22.2 mwaka wa fedha 2021/22 hadi kufikia sh. tril. 27.6 mwaka wa fedha 2023/2024 na kuvunja rekodi ya kukusanya sh. trilioni 16.528 katika kipindi cha Nusu Mwaka wa Fedha 2024/2025 kinachoanzia Julai hadi Desemba Mwaka 2024.
Dkt. Nchemba alitoa pongezi hizo, wakati akifungua Kikao Kazi cha siku 5 kinacho Tathmini Utendaji kazi wa Nusu Mwaka wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025, kinachofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano Arusha (AICC), Jijini Arusha.
Dkt. Nchemba aliitaka TRA kuimarisha zaidi mifumo ya kisasa ya kielektroniki ya kukusanya mapato ya Serikali ili kuongeza uwazi, tija na ufanisi kwa kukusanya mapato pamoja na kuziba mianya ya maafisa wa TRA kukutana uso kwa uso na walipakodi.
Dkt. Nchemba alitumia wasaa huo pia kuwataka wafanyabiashara kuacha tabia ya kukwepa kulipa kodi, kutumia ipasavyo mashine za kukusanya mapato ya Serikali (EFDs) na kuwahimiza watoe risiti halali zinazoendana na thamani ya manunuzi yaliyofanyika huku wananchi kwa upande wao wakihimizwa kudai risiti halali wanaponunua bidhaa na huduma mbalimbali.
Kwa upande wake, Kamisha Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, Bw. Yusuph Juma Mwenda, alisema kuwa Kikao kazi hicho, pamoja na mambo mengine, kilikuwa na malengo kadhaa ya kuimarisha ukusanyaji wa kodi ili kufikia malengo waliyowekewa na Serikali ya kukusanya shilingi trilioni 30.449 katika Mwaka wa Fedha 2024/2025.
Bw. Mwenda alisema kuwa mafanikio hayo yanatokana na TRA kuendelea kuhamasisha ulipaji kodi wa hiari, kuwasikiliza walipakodi na kutatua changamoto zao hatua iliyochangia kukua kwa uhusiano kati ya Mamlaka na walipakodi hususan kupitia viongozi wa vyama vya wafanyabiashara wote nchini wanaoendelea kuunga mkono kwa vitendo juhudi zinazofanywa na Serikali baada ya maelekezo ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuboresha mazingira ya biashara na ulipajikodi nchini.
Aliwahimiza watumishi wa TRA kuendelea kufanyakazi kwa bidii, juhudi na maarifa ili kufanikisha malengo ya Serikali ya kukusanya mapato yake kupitia kodi mbalimbali pamoja na kuzingatia weledi wanapotekeleza majukumu yao wakati Serikali kwa upande wake ikiendelea kuwajengea mazingira mazuri ya kufanyakazi.
Mwisho.