Site icon A24TV News

MAKAMU WA RAIS DKT PHILIP MPANGO ASISITIZA MFUMO WA UTOAJI TAARIFA KUTUMIKA KATIKA TAASISI ZOTE ZA UMMA .

Na Geofrey Stephen Arusha .

MAKAMUwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa rai kwa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kukamilisha mchakato wa kusanifu na kujenga Mfumo Mkuu wa Ubadilishanaji Taarifa Serikalini na kuhakikisha Taasisi zote za umma zinajumuishwa katika mfumo huo.

Makamu wa Rais ametoa rai hiyo wakati wa Ufunguzi wa Kikao Kazi cha Tano cha Mamlaka ya Serikali Mtandao kinachofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC). Amesema Jambo hilo ni muhimu ili kurahisisha utendaji kazi katika taasisi na kurahisisha utoaji huduma kwa wananchi kama ilivyoelekezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Taasisi za Umma kuhakikisha kuwa mifumo yao inasomana na kubadilishana taarifa..

Aidha Makamu wa Rais amesema Taasisi zote za umma zinapaswa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao katika hatua zote za ujenzi au ununuzi, usimamizi na uendeshaji wa Miradi ya TEHAMA pamoja na kuwataka kuwaelekeza Wakuu wote wa taasisi za umma kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo inayotolewa na Mamlaka husika katika utekelezaji wa shughuli za Serikali Mtandao.

Hali kadhalika, Makamu wa Rais ameagiza mikoa ambayo bado haijaanza kutumia utaratibu wa Ofisi ya Kielektroniki (e-office) kuhakikisha wanaaanza kutumia mfumo huo ifikapo tarehe 30 mwezi juni. Aidha ameagiza kituo cha utafiti kiweze kuimarishwa pamoja na kuongezewa eneo la ufanyaji kazi.

Makamu wa Rais amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika kuwajengea uwezo wataalamu wa TEHAMA na kada nyingine, kwa kuweka mazingira wezeshi ya ufundishaji katika Vyuo Vikuu na Taasisi za elimu ya juu ili viendelee kuzalisha wataalam wa kutosha.

Makamu wa Rais amewasihi washiriki wa kikao kazi hicho pamoja na Watanzania wote kwa ujumla, ambao wana sifa za kupiga kura kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa kuhakikisha wanajiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na kushiriki kupiga kura ili kuchagua viongozi wenye sifa na uwezo stahiki wa kusimamia na kuratibu shughuli za maendeleo katika ngazi husika.

Kwa upande wake Waziri Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene amesema lengo la kikao hicho ni kuwakutanisha wadau mbalimbali wa serikali mtandao kutoka katika Taasisi na Mashirika ya Umma na Sekta binafsi ili kuwapa fursa ya kujadili hatua iliyofikiwa katika jitihada ya serikali mtandao. Amesema kikao hicho kitaangazia mafanikio yaliyopatikana na changamoto zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa jitihada hizo na namna ya kukabiliana nazo.

Aidha ameongeza kwamba Tanzania imepiga hatua na kupata mafanikio katika utoaji huduma ambapo ilipata ushindi wa nafasi ya pili barani Afrika katika Ripoti ya utafiti ya Benki ya Dunia (2022) katika nchi 198 duniani, kuhusu Ukomavu wa Matumizi ya Teknolojia Duniani katika Utoaji wa Huduma za Serikali na Ushirikishwaji wa Wananchi (GovTech Maturity Index).

Awali akitoa taarifa ya kikao hicho Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi Benedict Ndomba amesema kuanzishwa kwa mamlaka hiyo kumeiwezesha serikali kuwa na udhibiti wa moja kwa moja wa mifumo na miundombinu ya TEHAMA inayotumika serikalini pamoja na kulinda usalama wa taarifa za serikali. Amesema Mamlaka ya Serikali Mtandao hutoa msaada wa kiufundi na ushauri kuhusu usalama wa TEHAMA na viashiria vya matishio ya kiusalama mtandaoni kwa Taasisi za Umma pamoja na kukabiliana na mashambulio ya kimtandao pindi yanapojitokeza.

Kikao hicho kinashirikisha zaidi ya washiriki 1300 ambapo Kauli mbiu ya kikao kazi hicho ni “Jitihada na ubunifu wa Serikali Mtandao kwa utoaji wa huduma za umma kwa ufanisi

Mkuu wa Mkoa wa Arusha poul Makonda amesema kutakuwa na michezo kama mpira wa miguu, ukiwahusisha wachezaji wa kike kutokataadhimishwa Kitaifa mkoani humo Machi 8, 2025 itakuwa ya kitofauti kwa kuwa wameandaa matukio mbalimbali.

Mhe. Makonda amesema hayo wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha tano cha Serikali mtandao, kinachofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), ambapo mgeni rasmi ni Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango.
Amesema kutakuwa na siku saba ambapo mambo mbalimbali yatafanyika na tukio hilo limepewa jina la ‘Wiki ya Wanawake’.

“Sherehe ya Siku ya Wanawake Kitaifa Arusha tunafanya kitu cha tofauti, haitakuwa tu tarehe 8 kama ilivyozoeleka. Mkoa wa Arusha tumekubaliana kuanza sherehe zetu tarehe 1 Machi, ambapo tutakuwa na siku saba za Wiki ya Mwanamke. Tumeomba wizara nane, na kazi ya kwanza itakuwa kutoa huduma,” amesema Makonda.

Mwisho .