Na Geofrey Stephen Arusha
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya umishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene ,ameitaka Mamlaka ya Serikali Mtandao e-GA kuendelea kufanya tafiti li kuleta bunifu kwa mifumo ya Tehama katika kuboresha utendaji kazi na kusaidia kuondoa kero ya upatika naji wa huduma mbalimbali za serikali kwa wananchi.
Waziri ameyasema hayo leo februali 13,2025 wakati wa kufunga Kikao Kazi cha 5 cha Serikali Mtandao e-ga kilichofanyika kwa muda wa siku tatu katika ukumbi wa AICC jijini Arusha na kuhudhuriwa na wadau takribani 1500 wakiwemo Maafisa Masuuli, Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo vya TEHAMA, Maafisa TEHAMA na watumiaji wengine wa mifumo ya TEHAMA kutoka katika Taasisi, Halmashauri na Mashirika mbalimbali ya Umma.
Waziri Simbachawene amesema Serikali imedhamiria kuimarisha na kuongeza matumizi TEHAMA ili kwenda sambamba na maendeleo ya Sayansi na Teknolojia kwa kuwa shughuli nyingi duniani ikiwemo za kiuchumi kwa sasa zinafanyika kwa kutumia TEHAMA.
Simbachawene amesema Serikali imetoa kipaumbele kwenye matumizi ya TEHAMA, hususani katika masuala ya utafiti na ubunifu, ili kuimarisha usalama wa Mtandao wa Mawasiliano na kuongeza watumiaji wa internet.
Alisema Wizara kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), imejipanga kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma mtandao kwa umma kidijitali sambamba na kuboresha upatikanaji wa mawasiliano ya simu nchi nzima, ili kuwawezesha Watanzania kupata huduma kwa wakati na kwa gharama kupitia mifumo ya TEHAMA,
‘Tunajivunia kuona idadi ya watumiaji wa simu za mkononi pamoja na internet, inaongezeka mwaka hadi mwaka. Ongezeko hili linatupa chachu ya kuboresha upatikanaji wa huduma za Serikali kupitia simu za mkononi na linadhihirisha ongezeko la matumizi ya TEHAMA hapa nchini.”
Waziri Simbachawene amezitaka taasisi za umma kuchukua hatua za haraka ili kuhakikisha zinatumia fursa ya ongezeko hili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi kidijitali kupitia simu za mkononi
Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Ikulu,Mulula Mahendeka amesema Vikao vinavyofanyika vimekuwa na manufaa makubwa katika kukuza na kuendeleza jitihada za Serikali Mtandao, kupitia mawazo mbalimbali yanayotolewa na washiriki wa vikao,
Mahandeka amesema Wizara, itasimamia utekelezaji wa maazimio yote yaliyofikiwa kwenye kikao hiki kwa wakati, ikiwa ni kwa Wizara yenyewe, e-GA au taasisi nyingine ya umma inayohusika.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao, Benedict Ndomba aliwashukuru washiriki wote kwa umakini, utulivu na usikivu walioonyesha wakati wote wa kikao, hali ambayo imechangia kupata mawazö bora wakati wa majadiliano.
Alisema mawazo yaliyotolewa ni chachu katika maendeleo ya Serikali Mtandao, na Mamlaka itayafanyia kazi maoni na mapendekezo yote yaliyotolewa kwa kuwa na jitihada za Serikali Mtandao zenye tija zaidi.
Ndomba alisema mawazo jumuishi katika utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao ni chachu ya kuongeza ufanisi katika utendaji kazi na upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi kidijitali, ili kuwezesha upatikanaji wa huduma hizo kwa urahisi, haraka na kwa gharama nafuu,
Mwisho.