Na Doreen Aloyce,Dodoma
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imejipanga vyema kukamilisha maandalizi yote muhimu ikiwemo miundombinu kwa ajili ya Michuano ya Mpira wa Miguu kwa Nchi za Africa CHAN na AFCON.
“Tanzania imejipanga vizuri, kuhakikisha kuwa michuano hii inafanyika hapa Nchini, Serikali inawajibika kuhakikisha inaandaa viwanja na miundombinu mingine.”
Ameyasema hayo jijini Dodoma aliposhiriki katika Tamasha la Michezo la Bunge Bonanza lililofanyika kwenye Viwanja vya Shule ya Sekondari ya John Merlin jijini Dodoma.
Amesema kuwa tayari ukaguzi wa baadhi ya viwanja umefanyika na vimeonekana kukidhi vigezo “Viwanja vilivyokaguliwa vipo Tanzania bara na Visiwani, na kazi bado inaendelea, lengo ni kuhakikisha michuano hii inafanyika kwa ufanisi”
Mheshimiwa Majaliwa amesema ni vyema sasa Watanzania wakajipanga kutumia fursa zitakazo jitokeza kutokana na kuwepo kwa michuano hiyo hapa Nchini. “Hii ni fursa kwetu Watanzania, lazima tujipange kutumia fursa za kiuchumi zitakazojitokeza, ili tuweze kunufaika”.
Aidha, Mheshimiwa Waziri Mkuu amempongeza Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson kwa kuandaa Tamasha la Michezo la Bunge Bonanza ambalo limewakutanisha wabunge na wanamichezo mbalimbali wa Mkoani Dodoma.
“Tamasha hili limekuwa na mafanikio makubwa, limetupa nafasi wabunge kufanya mazoezi na kushiriki michezo mbalimbali pamoja na kuimarisha afya zetu.”
Amesema ni vyema Watanzania wakaendelea na utamaduni wa kufanya mazoezi ili kuimarisha afya zao.
Wabunge mashabiki wa Simba na Yanga kuzichapa kesho,kuchuana kesho
Mawatambiana kila mmoja kumshinda mwenzake viwanja vya John Merin Dodoma
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Tulia Akson ni utaratibu wao kufanya bonanza la Michezo mbalimbali ambalo huwa litawakutanisha wabunge, watumishi wa Bunge, na mashabiki wa michezo.
Bonanza hili huwa linalenga kuhimiza watu kufanya mazoezi mara kwa mara ili kuepuka magonjwa yasiyoambukiza na kupunguza mzigo wa matibabu kwa jamii pamoja na kujenga mahusiano bora.
Mwenyekiti wa Bunge Bonanza, Festo Sanga, amesema bonanza hili limeendelea kukua na mwaka huu watu wengi wamejitokeza na kushiriki michezo mbalimbali.
“Tunataka kuona watu wakichangamkia fursa ya kufanya mazoezi ili kuboresha afya zao, Pia, tunalenga kuimarisha mahusiano kati ya wabunge na watumishi wa Bunge kupitia michezo, ”
Katika kuhakikisha bonanza linakuwa la mafanikio, waandaaji wake wamepanua wigo wa ushirikiano kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, zikiwemo taasisi za serikali na binafsi kama DUWASA na Hospitali ya Benjamin Mkapa.
Meneja wa Azania Bank Tawi la Dodoma, Laiberia Peter, amesema benki hiyo imefadhili bonanza hilo kwa kutoa vifaa vya michezo, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha mazoezi na kuchochea afya na wataendelea kushirikiana na Bunge.
Hata hivyo bonanza hilo liliambatana na tuzo na medali mbalimbali.
Mwisho.