Site icon A24TV News

WAZIRI GWAJIMA AFIKA ARUSHA AFURAISHWA NA MAANDALIZI KUELEKEA KILELE CHA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI

Na Geofrey Stephen Arusha .

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum, Dkt. Doroth Gwajima ameupongeza Mkoa wa Arusha kwa maandalizi mazuri kuelekea wiki ya wanawake duniani, akihimiza jitihada zaidi kwenye utekelezaji wa mikakati ya kuwainua wanawake katika nyanja mbalimbali pamoja na kuondoa unyanyasaji na ukatili kwa wanawake na wasichana.

akizungumza na wajumbe wa kamati mbalimbali za maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya mwanamke duniani Machi 08, 2025, Waziri Dkt. Doroth Gwajima amesisitiza pia umuhimu wa Mkoa wa Arusha na mikoa mingine kote nchini, kuendelea kutoa elimu ya afya, Mikopo kwa wanawake sambamba na kuwafahamisha wananchi kuhusu fursa za uwezeshaji wanawake kiuchumi.

Akikemea udhalilishaji na ukatili wa kijinsia unaotokana na baadhi ya tamaduni katika Mikoa ya Arusha na Manyara inayopelekea ukeketaji kwa wasichana, Dkt. Gwajima amesisitiza umuhimu wa kubuniwa mikakati mbalimbali ya kutokomeza ukatili huo ili kubadilisha sura na takwimu za unyanyasaji katika Mikoa hiyo pamoja na kutokomeza fikra na tamaduni za kale zisizokuwa na faida kwa zama hizi.

Katika mazungumzo yao, Mhe. Makonda ameeleza kuwa Mkoa wa Arusha upo tayari kwaajili ya Siku ya mwanamke duniani ambapo maadhimisho yake Kitaifa yanatarajiwa kuwa Machi 08, 2025 Jijini Arusha na Kuongozwa na mgeni rasmi Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisema katika Juma la kuelekea Machi nane, shughuli mbalimbali zitafanyika ikiwemo elimu mbalimbali na utoaji wa elimu na msaada wa kisheria kwa wasichana na wanawake wa Mkoa wa Arusha pamoja na mashindano ya michezo ya aina mbalimbali kwaajili ya wanawake kando ya burudani nyingine zitakazotolewa na wanawake ikiwemo mbio za magari na muziki kutoka kwa wanawake wanaounda bendi mbalimbali.

Kikao hicho pia kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano kwenye Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Arusha, kilihudhuriwa na washauri wa Rais Mhe. Angellah Kairuki pamoja na Mhe. Sophia Mjema, Katibu tawala Mkoa wa Arusha Musa Missaile, wadau mbalimbali kutoka Taasisi za kifedha na wa masuala ya wanawake pamoja na Viongozi wengine wa Chama Cha Mapinduzi CCM na serikali.

Mwisho .