Na Joseph Ngilisho -ARUSHA
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA)imesema inaunga mkono kampeni ya serikali ya matumizi sahihi ya nishati safi na salama kwa kurahisisha utoaji wa vibali na kuwaomba wawekezaji kuchangamkia fursa hiyo ili kuwasogezea huduma wananchi hususani waishio vijijini.
Hayo yamebainishwa leo Machi 6,2025 na Afisa Mkuu- Uchambuzi wa mahesabu na fedha (EWURA),Herierh Kasilima wakati akiongea na vyombo vya habari katika banda la maonyesho la EWURA lililopo jijini hapa ,katika kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ambayo kitaifa yanafanyika jijini Arusha,Machi,8,2025.
Kasilima ambaye pia ni mwenyekiti wa wanawake Tughe ,tawi la EWURA alisema katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani wamekuwa chachu katika kuhamasisha matumizi sahihi na salama ya nishati ya kupikia na kuwataka wawekezaji wa nishati kuchangamkia fursa hiyo.
“Sisi kama Ewura tumejipanga kuhamasisha wanawake kutumia nishati safi ya kupikia kwa kutoa elimu kwa umma hususani wanawake ambao ndio watumiaji wakubwa wa nishati ya kupikia LPG”
Alisema Ewura imekuwa ikihamasisha wawekezaji wa nishati kwenda kuwekeza nishati ya umeme ama gesi ya kupikia majumbani(LPG) katika maeneo ya umma baada ya kurahisisha utoaji wa vibali,hatua ambayo itasaidia wananchi kupata huduma hiyo na kuondokana na athari zinazotokana na matumizi ya kuni.
“Tumewezesha upatikanaji wa gesi asilia ,masuala ya bei na vibali vya uwekezaji ,vyote hivyo vinamfanya mwanamke kuweza kupata nishati kwa urahisi zaidi na kuweza kuitumia ili kuondokana na madhara ya utumiaji wa gesi isiyo salama”
“Tunachotaka sisi kama Ewura wanawake wahamasike kutumia gesi Asilia ama umeme jambo ambalo litasaidia kuokoa muda pamoja na utunzaji wa mazingira”Alisema
Naye Mhandisi Mkuu wa Umeme Ewura,Mwanamkuu Kanizio alisema Ewura imejipanga kusherehekea maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani kwa kutoa elimu na kuhamasisha makundi mbalimbali ya wanawake ili kuelewa dhima nzima ya matumizi ya nishati safi ya kupikia .
Alisema Ewura imekuwa ikisimamia upatikanaji wa nishati safi pamoja na viwango bora vya LPG na matumizi sahihi ya nishati safi inayotumiwa na mlaji pamoja na kuhakikisha bei anayo pata mlaji ni himilivu.
“Ewura inasimamia shughuli za uagizaji,uhifadhi na usambazaji wa gesi ya kupikia LPG zinatakiwa zifanywe kwa namna ambavyo inazingatia misingi ya usalama na viwango.Lengo ni kukidhi mahitaji ya afya ,usalama na mazingira kwa watu na mali zao”
Ends..