Na Geofrey Stepheb Arusha .
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay, ameeleza kuwa mwaka wa fedha 2024 umeweka msingi imara wa utekelezaji wa Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Benki, unaolenga kuboresha huduma na kupanua wigo wa utoaji huduma ili kuwafikia wateja wengi zaidi nchini na nje ya mipaka.
Akiendelea kufafanua, Dkt. Laay amesema kuwa licha ya changamoto mbalimbali, Benki imeendelea kufanya vizuri na kufanikisha malengo kadhaa ya kimkakati katika mwaka huu wa fedha, ikiwa ni mwaka wa pili tangu kuanza kutekelezwa kwa Mpango Mkakati wa muda wa kati. Mafanikio haya yamechochewa na uwekezaji madhubuti kwenye mifumo ya kidijitali, ubunifu wa bidhaa, pamoja na kuimarishwa kwa uzoefu wa wateja.
Aidha, Dkt. Laay ameeleza kuwa Bodi ya Wakurugenzi inaendelea kuhakikisha inapata uwiano sahihi kati ya kuongeza thamani kwa wanahisa na kuwekeza kwenye maeneo yenye fursa za kukuza ustawi wa Benki kwa muda mrefu. Kwa kuzingatia mafanikio yaliyopatikana mwaka huu, Bodi inapendekeza gawio la shilingi 65 kwa kila hisa moja kwa mwaka wa fedha ulioishia tarehe 31 Desemba 2024, kiasi kinachofanya jumla ya gawio kufikia takribani shilingi bilioni 169.9.³
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, amesema kuwa utekelezaji makini wa Mpango Mkakati wa muda wa kati wa miaka mitano umeendelea kuzaa matunda makubwa, ambapo kwa mwaka wa fedha 2024, Faida Baada ya Kodi (PAT) ilikua kwa 30.3% na kufikia Shilingi bilioni 551, kutoka Shilingi bilioni 422.8 mwaka 2023.
Amesema mafanikio haya yanadhihirisha uimara wa mikakati ya Benki pamoja na nafasi yake kama taasisi inayoongoza katika sekta ya huduma za kifedha nchini na ukanda wa Afrika Mashariki. Aidha, mizania ya Kundi imeongezeka kwa kiasi kikubwa na kufikia Shilingi trilioni 16.7, kutoka Shilingi trilioni 13.3 mwaka 2023, ikiwa ni ongezeko la takribani 25.6%, linalotokana na mikakati madhubuti ya uwekezaji na uendelezaji wa biashara.
Akizungumzia juhudi za kukuza ujumuishi wa kifedha, Nsekela amesema Benki imeendelea kuwawezesha wateja wa kada mbalimbali ikiwa ni pamoja na wajasiriamali, biashara ndogo na za kati, pamoja na wawekezaji katika sekta ya viwanda. Kupitia programu ya IMBEJU inayoendeshwa na CRDB Bank Foundation, vijana na wanawake wengi wamepata fursa ya kujiendeleza kiuchumi.
Kwa mwaka wa fedha 2024, Benki pia imeongeza nguvu katika ushirikiano wa kimkakati kwa ajili ya kufadhili miradi mikubwa ya maendeleo, hususan kwenye sekta za miundombinu, nishati, na kilimo. Akiangazia siku za usoni, Nsekela amesema Menejimenti itaendelea kuimarisha mchango wa kampuni tanzu, kuboresha huduma kwa wateja, na kuwekeza zaidi kwenye mifumo ya ubunifu wa kidijitali.
Kadhalika, amesema Benki itaendelea kuimarisha usimamizi wa vihatarishi, kuhakikisha utawala bora, na kujiimarisha zaidi .
Mwisho .