Site icon A24TV News

NAIBU WAZIRI MKUU DOTO BITEKO ARIDHISHWA NA MRADI MKUBWA WA KITUO CHA MAJI CHEKERENI ARUSHA APONGEZA AUWSA

Na Geofrey Stephen Arusha .

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Arusha (AUWSA), Mhandisi Justine Rujomba, amesema mafanikio makubwa yaliyopatikana katika upatikanaji wa huduma ya maji safi na usafi wa mazingira ni matokeo ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya Shilingi bilioni 520, unaofadhiliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

Akizungumza  leo april 26, 2025, wakati wa ziara ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Mashaka Biteko, katika kituo cha kusambaza maji cha AUWSA kilichopo Chekereni, wilayani Arumeru,

Mhandisi Rujomba alisema Rujomba alibainisha kuwa hadi sasa, kiwango cha upatikanaji wa maji katika maeneo yanayohudumiwa na AUWSA kimefikia asilimia 99.2 – zaidi ya lengo la Serikali la kufikia asilimia 95 ifikapo mwaka 2025. Aidha, muda wa upatikanaji wa huduma umeongezeka kutoka saa 16 kwa siku mwaka 2020 hadi saa 22 mwaka 2025, huku idadi ya wateja waliounganishwa ikiongezeka kutoka 71,183 mwaka 2021 hadi 134,000 kwa sasa.

Katika sekta ya usafi wa mazingira, AUWSA imeongeza mtandao wa ukusanyaji majitaka kutoka asilimia 8.03 mwaka 2020/21 hadi asilimia 39.5 mwaka 2024/25. Imepata pia magari matano ya kisasa ya kunyonya majitaka yenye uwezo wa kubeba kati ya lita 5,000 na 10,000. Mabwawa ya kutibu majitaka yaliyopo Kata ya Terati yameboreshwa na sasa yana uwezo wa kutibu lita milioni 22 kwa siku, kutoka lita milioni 3.5 hapo awali.

Dkt. Biteko, akizungumza baada ya kutembelea kituo hicho, aliipongeza AUWSA kwa mafanikio hayo akisema:

“Niwapongeze kwamba kiwango cha maji mnachozalisha ni kikubwa kuliko mahitaji. Manake ni kwamba upatikanaji wa maji umefika asilimia 99. Hii ni hatua kubwa sana.”

Hata hivyo, Naibu Waziri Mkuu alieleza wasiwasi wake kuhusu kiwango kikubwa cha upotevu wa maji:

> “Kwa mujibu wa taarifa ya EWURA, asilimia 49 ya maji yanapotea kabla hayajafika kwa wateja. Kwa kuwa uko kwenye eneo lenye wateja wengi, hakikisha unatafuta suluhisho la kudhibiti upotevu huu,” alisisitiza.

Dkt. Biteko pia alihimiza umuhimu wa kuwa na vyanzo mbadala vya nishati kwa ajili ya kuendesha pampu za maji, akieleza kwamba kukatika kwa umeme kunaweza kuathiri moja kwa moja upatikanaji wa huduma hiyo muhimu:

Pamoja na mafanikio hayo, Dkt. Biteko alitoa rai kwa AUWSA kushughulikia malalamiko ya wananchi kuhusu bili zisizolingana na matumizi:

> “Mkiona wananchi wanalalamika kuwa bili ni kubwa kuliko matumizi, hilo ni jambo linalowahusu moja kwa moja. Hakikisheni mnalidhibiti,” alieleza.

Kwa mujibu wa Rujomba, maeneo yanayohudumiwa na AUWSA ni pamoja na Jiji la Arusha, Monduli, Ngaramtoni, USA River, Mererani, na Longido – likijumuisha kata za Namanga na Kimokou – kwa jumla ya wakazi zaidi ya milioni 1.07 kulingana na sensa ya mwaka 2022.

Mradi huo mkubwa umehusisha uboreshaji wa mfumo wa maji safi, uondoaji wa majitaka, pamoja na uimarishaji wa uwezo wa kitaasisi. AUWSA imejenga mtambo wa kutibu maji katika chanzo cha Midawe unaoweza kutibu lita milioni 10 kwa siku, ofisi kuu katika eneo la Safari City, pamoja na ofisi nne za kanda.

> “Kwa sasa tunaweza kusema AUWSA ndiyo mamlaka ya kwanza nchini yenye mabwawa ya kisasa na yenye uwezo mkubwa wa kutibu maji taka. Pia tumefanikisha uchimbaji wa visima 56, viwili kati ya hivyo vikitoa maji kwa nguvu ya asili bila kutumia mashine – jambo linalosaidia wananchi kuendelea na shughuli za kilimo hata visima vikubwa visipofanya kazi,” alisema Rujomba.

Akihitimisha ziara yake, Dkt. Biteko alisisitiza umuhimu wa matumizi sahihi ya fedha zilizowekezwa katika mradi huo:

“Fedha zilizowekwa hapa ni nyingi mno – zaidi ya bilioni 500. Ni lazima fedha hizi zitafsiri maisha bora ya watu. Maisha hayawezi kuwa bora kama hakuna maji. Maji hayana mbadala.”

Mwisho