Arusha
Jumla ya walimu 220 kutoka shule mbalimbali Wilayani Karatu iliyoko Mkoani Arusha wamefikiwa na elimu ya kifedha kutoka kwa maofisa waandamizi wa benki ya NMB.
Walimu hao wamepata elimu hiyo Leo julai 14,2025 chini ya mpango wa ‘mwalimu Spesho’ unatekelezwa na NMB kwa ajili ya kuwasaidia walimu katika nidhamu ya matumizi ya kifedha na fursa za uwekezaji kwa ajili ya ustawi wa uchumi wao na taifa kwa ujumla.
Meneja mwandamizi wa idara ya wateja binafsi kutoka NMB makao makuu, Ally Ngingite amesema walimu hao wanaungana na wengine zaidi ya 120,000 nchini waliofanikiwa kupata elimu hiyo.
Lengo ni kuhakikisha walimu hawateseki tena na masuluhisho ya kifedha hasa uwekezaji isiyo na faida na na mikopo kausha damu.
Amesema kuwa kwa miaka 10 tangu kuanzishwa kwa mpango huo zaidi ya walimu 120,000 wamefikiwa na elimu hiyo inayowajengea nidhamu ya matumizi ya kifedha, kuwaonyesha fursa za uwekezaji kwa fedha zao au mikopo inayotolewa na NMB.
“Lakini pia tunatoa elimu ya suluhu za changamoto zao mbalimbali za kifedha kwa ajili ya ustawi wao wa kiuchumi wa sasa na baadae wakistaafu”
Amesema ndani ya kongamano hilo, pia wanawapa walimu elimu ya jinsi ya kujiandaa kustaafu kwa uchumi endelevu lakini pia maswala ya afya ya akili.
Akifungua kongamano hilo, Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Karatu Juma Hokororo amesema kuwa walimu wamekuwa waathirika wakubwa wa mikopo umiza na kuishukuru benki ya NMB kwa kuwafikia walimu wa Karatu na elimu hiyo.
“Elimu ya kifedha nadhani ndio ilikuwa tatizo, ndio maana matapeli walikuwa wanawatesa, sasa tumieni fursa hii ya Elimu na mikopo kuhakikisha mnachukua hatua mpya ya maisha na ustawi wa uchumi wenu” amesema.
Amewataka walimu hao kuepuka mikopo yenye masharti ya kuwadhalilisha na kushusha heshima ya taaluma yao ikiwemo inayotaka dhamana ya kadi ya benki wanayotumia kulipwa nazo mishahara.
Amewataka kuchukua mikopo hiyo katika taasisi zilizo rasmi na zinazotambulika lakini pia wazingatie masharti yake.
“Mikopo ya hovyo hovyo wala haiwezi kuwasaidia kiuchumi zaidi inawadidimiza kwa kuwafilisi mnaposhindwa kulipa, hivyo kuanzia sasa hivi anzeni kuzingatia taasisi zenye heshima na hadhi”
Ametumia nafasi hiyo kuipongeza benki ya NMB kwa huduma mbalimbali wanazotoa kusaidia serikali katika sekta ya afya, elimu na mazingira .
Nae Meneja wa NMB wilaya ya Karatu, Edgar Ninga, amesema kuwa elimu hiyo pia inawasaidia walimu kujua masuluhisho yao ya kifedha za kidigitali zinazotolewa na taasisi hiyo ili waweze kujihudumia mkononi bila ya kufuata Ofisi.
Mmoja wa walimu kwenye kongamano hilo, Matilda Mathiasi kutoka shule ya Karatu Sekondari amesema kuwa elimu hiyo ni muhimu kwao na itawasaidia kutatua changamoto mbalimbali za kifedha wanazopitia walimu nchini.
Mwisho