Na Richard Mrusha Geita
WAZIRI wa Madini Antony Mavunde amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais DKT. Samia Suluhu Hassan itaendelea kusimamia sheria ya Local contect ili kuhakikisha watanzania wananufaika na rasilimali zao ikiwemo madini ya dhahabu .
Mavunde ameyasema hayo alipotembelea mmoja wa wawekezaji wa wazawa mkoani Geita Athanas Inyasi anaemiliki kampuni ya blue coast ili kujionea namna alivyonufaika na sheria ya Local contect ambapo amewasisitiza wafanyabiashara ,wachimbaji kujitokeza kuomba zabuni .
“Kwa hiyo nitoe rai kwa makampuni mengine yakitanzania kuchangamkia fursa hii sisi kama serikali tutahakikisha tunaisimamia sheria hii vizuri ili watanzania wengi zaidi waweze kunufaika tunahitaji kuwaona akina mzee Inyasi wengi zaidi kama alivyomsema mkuu wa Mkoa ili mwisho wa siku tuweze kuyaona matokeo ya uchumi wa madini katika maisha ya watanzania na kupitia uchumi huu tuweze kukuza pia uchumi wa tanzania na jambo hili linawezekana”,amesema Mavunde.
Aidha Waziri Mavunde amesema kuwa uwekezaji wa kampuni ya blue cost umesaidia kutoa ajira nyingi kwa vijana wakitanzania pamoja na kuchangia mapato ya halmashauri pamoja na kodi ya Serikali hivyo uwepo wake una maana kubwa katika maendeleo ya nchi na hususani mkoa wa Geita.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Makampuni ya Blue Cost ,Athanas Inyasi amesema uwepo wa sheria ya local Contect imesaidia kwa kiasi kikubwa kutokana na kuleta mafanikio makubwa kwa watanzania,huku ajira 360 zikiwa zimetolewa na kampuni hiyo.
“Ninapenda nimshukuru kwa namna ya pekee Rais wa Tanzania mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan anavyoendele kutuwekea mazingira mazuri sisi wafanyabiara na wananchi wote kwa jumla na mambo yetu yakaweza kuendelea kukua kitaifa na kimataifa”amesema Inyasi.
Awali akitoa taarifa fupi ya mradi huo Mkurugenzi Mtendaji wa Blue Coast Ndahilo Athanas amesema kampuni yao imejikita pia katika kujenga miundo mbinu ya maendeleo kama madarasa na madawati kwa shule za msingi Nyamalembo na Mseto zilizopo mkoani Geita wakiwa na lengo lakuangalia na sekta nyingine hasa sekta ya afya kwa siku chache za mbeleni.
“Mheshimiwa Waziri kwa kuzidi kutambua umuhimu wa sekta ya elimu kampuni yetu imetoa mchango wa shilingi milion 150 kupitia mfuko wa GPE Multplier Grant kwa ajili ya uboreshaji wa elimu katika shule za msingi yenye lengo lakutatua changamoto za walimu nchini “amesema Ndahilo
Naye Mkuu wa Mkoa wa geita,Martine Shigela ametumia nafasi hiyo kuwataka wachimbaji wadogo pindi wanapopata fedha waweze kubadilisha biashara ambazo zitawaongezea kipato.
Aidha amesema uwepo wa Local Contect umeongeza kwa kiasi kikubwa ajira kwa watanzania na kutoa fursa za wazawa kupata manufaa kutokana na shughuli ambazo zinafanyika kwenye maeneo yao.
Aliongeza kuwa watahakikisha watanzania wananufaika na rasilimali za nchi ikiwemo madini ya dhahabu
Mwisho