Na Joseph Ngilisho ARUSHA
Wananchi na wakazi wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini wameshauriwa kujitokeza kwa wingi kupima na kupata tiba ya Magonjwa ya Moyo katika Hospitali ya Rufaa ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC)baada ya kubainika kuwa watu wengi wenye matatizo hayo wanatoka ukanda wa kaskazini hususani mikoa ya Arusha na Manyara.
Rai hiyo imetolewa na Daktari Bingwa na Bobezi wa Magonjwa ya Moyo Kutoka hospitali ya taifa ya Jakaya Kikwete (JKCI) dkt Samweli Rweyemamu,wakati akiongea na waandishi wa habari katika hospitali ya ALMC jiiini Arusha na kusisitiza kuwa bado wanaendelea kutoa huduma ya matibabu ya moyo kwa wananchi wa ukanda Kaskazini.
Alisema kuwa magonjwa ya moyo kwa kanda ya kaskazini yamekuwa yakiongezeka hususani shinikizo la damu huku alisema inachagiwa zaidi na mfumo wa maisha unaochangiwa zaidi na kutofanya mazoezi na kuwataka wananchi kujenga tabia ya kupima afya zao.
Awali Mkurugenzi mtendaji wa hospitali ya ARUSHA LUTHERAN MEDICAL CENTRE ALMC, DKT GODWIL KIVUYO alisema kuwa hospitali hiyo itakuwa ikitoa huduma za Magonjwa ya moyo kwa kushirikiana na madaktari bingwa kutoka taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete .
Alisema hivi karibuni kulikuwa na kambi ya madaktari bingwa wa Moyo kutoka JKCI na baada ya kumalizika kwa kambi hiyo ya uchunguzi na matibabu ya moyo Madaktari hao wameendelea kuwepo na bado wanaendelea kutoa huduma hiyo katika hospitali hiyo ya ARUSHA LUTHERAN MEDICALCENTRE alimaarufu Seliani.
Dkt Kivuyo alisema kambi hiyo ilikuwa na mafanikio makubwa kwani mwitikio ulikuwa mkubwa ,wagonjwa zaidi ya 600 wamepatiwa huduma ya matibabu ya Moyo na baadhi yao walipelekwa kutibiwa katika hospitali ya Moyo ya jakaya Kikwete kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
“Tangu kambi imeisha madaktari wameendelea kutoa huduma ya matibabu ya moyo hapa katika hospitali yetu ya Arusha Lutheran Medical Centre wakishirikiana na madaktari bingwa kutoka hospitali ya Jakaya Kikwete “
Dkt kivuyo aliwashauri wakazi wa mikoa ya kaskazini kufika katika hospitali hiyo kuchunguza afya zao ili wakibainika kuwa na tatizo la moyo waweze kutibiwa mapema kwa gharama nafuu.
Ends.