Na Doreen Aloyce, Dodoma
Serikali imechukua hatua mbalimbali kutatua changamoto za kiuchumi katika vituo vya utangazaji nchini kwa kupunguza ada za leseni za mwaka kwa takribani asilimia 40.
Pia Serikali imepunguza ada za masafa ya utangazaji katika maeneo ambayo hayana tija kibishara.
Haya yameelezwa jijini hapa jana, Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia, Kundo Methew, wakati akifungua Mkutano Siku Mbili wa Nwaka wa Watao Huduma wa Sekta ya Utangazaji pamoja na Maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani.
“Hatua za kwanza Serikali iliyochukua ni kupunguza ada za mwaka za leseni utangazaji kwa takribani asilimia 40,” amesema Methew
Methew alisema, Serikali pia imepunguza ada za masafa ya utangazaji katika maeneo ambayo hayana tija kibishara.
Naibu Waziri huyo amesema hatua hiyo yote ni dhamira safi ya serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia kuhakikisha kwamba huduma za utangazaji zinaboreshwa.
“Kazi kubwa inayofanywa na Rais Samia ni kuhakikisha kwamba watoa huduma za utangazaji hasa redio zinazidi kuwa na tija katika uchumi wa vituo na taifa kwa ujumla”amesema Methew.
Amesema serikali pia imeunda kamati inayochunguza uchumi wa vituo vya utangazaji ili kupata hali halisi ya changamoto wanazopitia katika kutoa huduma.
“Matarajio ya serikali ni kwamba kamati hiyo itakuja na majibu sahihi yatakayowezesha serikali kuchukua hatua stahiki zitakazokidhi changamoto za kibiashara zinazokabili vituo hivyo,” amesema Methew.
Serikali ipo tayari wakati wowote kushirikiana na wadau wa utangazaji katika kuhakikisha kunakuwa na mazingira bora kisera na kibiashara katika uwezeshaji na utoaji huduma bora nchini.
Amesema Sekta ya utangazaji imekuwa ikipitia mabadiliko ya kiteknolojia ambayo kila wakati yanahitaji kurejea kanuni za utangazaji ili kwenda na hali halisi iliyopo kwenye soko.
“Historia ya redio na runinga nchini kwa takribani miaka 50 utangazaji wake ulitumia mitambo ya analogia. kwa runinga hadi mwaka 2010 nchi ilihama kutoka kutumia mitambo ya analogia na kwenda wa kidigiti,”amesema Methew
Na kuongeza kuwa “Safari hiyo ya utoaji huduma za utangazaji imekuwa ya mabadiliko, lakini vyanzo vya mapato vya kuendesha vituo vikiwa vile vile. Huduma ya utangazaji kwa kiasi kikubwa inategemea matangazo ya biashara na ufadhili wa vipindi kutoka kwa wafadhili”amesema Methew.
Mathew amesema jukwaa la intaneti limebadilisha huduma ya utangazaji duniani, kitendo cha watu kuhamia kwenye intaneti na kutumia simu za viganjani kupata matangazo, kumeleta ushindani ambao umeleta changamoto ya kuhakikisha uwanja katika utoaji huduma za utangazaji unakuwa sawia.
Akizungumzia Siku ya Redio Duniani alivitaka vyombo vya utangazaji nchini kuzingatia kaulimbiu, ‘Redio na Amani’ ili kuhakikisha kuwa maadhui wanayolisha wasikilizaji yanaendelea kuleta amani na umoja nchini.
Naibu waziri huyo amesema matangazo ya redio nchini yanatakiwa kufika mahali popote hasa yale maeneo ya pembezoni ili wananchi wanaoishi katika maeneo hayo waendelee kuwa sehemu ya jamii ya Tanzania.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Jabir Bakari amesema TCRA inasimamia sekta ndogo tatu ikiwemo mawasiliano ya simu na intaneti, utangazaji pamoja na posta na usafirishaji wa vipeto.
Bakari amesema mpaka kufikia Desemba 2022, TCRA katika sekta ndogo ya utangazaji zinawatoa huduma 787.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TCRA, Othman Sharif Khatib amesema kaulimbiu ya mkutano huo ni Mchango wa Sekta ya Utangazaji katika kukuza uchumi wa kidigatali, hivyo washiriki wa mkutano huo kama uwanja wa kubadilisha uzoefu na kuelewa fursa zilizopo katika uchumi wa kidigitali katika kuendeleza utangazaji wao.
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi za Mawasiliano Afrika Mashariki (EACO), Dk.Ally Simba amesema jumuiya imeunda kikosi kazi cha kuandaa mwongozo kuhusu upatikanaji wa redio na mwingiliano katika mipaka ya nchi saba za Afrika Mashariki.
Mwisho