Na Doreen Aloyce, Dodoma
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahman Kinana amewataka viongozi wa chama hicho kuyasemea mambo mazuri yanayofanywa na serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan katika maeneo yao.
Kinana ameyasema hayo jijini hapa jana,wakati akifungua Mfunzo ya siku mbili ya viongozi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kuanzia ngazi ya Taifa hadi Wilaya.
“Katika maeneo yenu hakikisheni mnakisemea chama na mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Dk.Samia,na wala msione haya kusema ili wananchi wajue na hata katika chaguzi zijazo tusipate shida.
Ameongeza kuwa:”Chini ya uongozi wa Rais Dk.Samia katika kipindi cha miaka miwili kila kata kuna alama ya maendeleo ameweka ikiwemo shule,zahanati,barabara na maendeleo ya watu hivyo tuna kila sababu ya kujisifia na kuusifia uongozi wa Mwenyekiti wa chama hiki.
Katika hatua nyingine Kinana amewataka UWT kubeba ajenda za wanawake kitaifa bila kuogopa jambo lolote.
Akizungumzia uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 Kinana amewataka wanawake kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ili kufia lengo la kujenga jamii ya usawa.
Amesema mwakani kuna uchaguzi wa viongozi wa serikai za mitaa, ni vyema wanawake wakajitokeza kuchukua fomu kwa ajili ya kuomba nafasi mbalimbali za uongozi na CCM itawapa ushirikiano wa kutosha.
“Kuelekea uchaguzi ujao jiandaeni na kuwahimiza wanawake kuwania nafasi zote za uongozi na ninawahakikishia kuwa CCM itawaunga mkono kwa hali na mali ili kuwa na wanawake wengi waliochaguliwa katika majimbo,”amesema
Katika hatua nyingine Kinana amewataka UWT kuhakikisha maamuzi mengi yanafanyika kupitia vikao na sio maamuzi ya mtu mmoja au kikundi cha watu.
Amesisitiza kuwa hata kiongozi anapokosea sio busara kumuamisha kituo cha kazi kabla ya kumuita na kumsikiliza kwani utakuwa ni ukiukwaji wa haki.
“Niwasihi tumieni vikao kuamua mambo sio makundi cha watu kila kitu lazima kijadiliwe kwa kina na kipite kwa hoja kwasababu ndani ya CCM hakuna maamuzi ya mtu mmoja au amri, na ninyi katika maeneo yenu hakikisheni ndani ya vikao huko ndio haki ya mtu itapatikana,”amesema
Kinana amewataka viongozi hao kuto wahamisha hovyo viongozi kwani amebaini wengine wanashtukizwa bila kupewa taarifa ya uhamisho.
“Wenyeviti mpunguze kuhamisha watu hovyo kama mtu amekosea aitwe aelezwe kosa sio kuchukua maamuzi ya haraka una mualibia mtu mwelekeo, tujenge utamaduni wa kuambiana ukweli na msiogopane mtu anapokosea ,”amesema
Makamu huyo amewashauri viongozi hao kusoma vitabu mbaimbali vya chama ikiweo Ilani ya uchaguzi,sera,kanuni katiba vitawasaidia katika masuala mbalimbali ya uongozi.
Amesema CCM ni miongoni mwa vyama vichache duniani ambayo vinamaandishi mengi.
“Someni katiba, kanuni, ilani, na sera vitawasaidia kuendesha shughuli mbalimbali za chama na kuongoza kwa kuzingatia mingi ya haki,”amesema.
Awali Mwenyekiti wa UWT Taifa Marry Chatanda amesema wanawake wanaridhika na kazi zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dk.Samia na ilani ya CCM inatekelezwa kwa kishindo.
Amesema katika kipindi cha miaka miwili ya serikali ya awamu ya sita hakuna kilichosimama ndio maana waliandaa hafla ya kumpongeza Rais Dk.Samia kwa kazi nzuri alizozifanya.
“Sisi wanawake wa CCM hakika tumeridhishwa na uongozi wa Rais Dk.Samia na tunaahidi katika uchaguzi wa mwaka 2025 tutatoa fedha kwa ajili ya kumchukulia fomu mwanamke mwenzetu,”amesema
Naye Katibu wa UWT Taifa Dk.Philis Nyimbi amesema lengo la mafunzo hayo ni kuleta ustawi na kuwapatia viongozi maarifa namna ya kuongoza jumuiya hiyo katika ngazi zote.
Amesema mafunzo hayo yamewakutanisha viongozi 478 ambapo baada ya kumaliza elimu waliyoipata wataipeleka katika ngazi ya kata na matawi.
“Mafunzo haya ni mahususi kwa ajili ya kuwajengea uwezo viongozi wetu ukizingatia tunaelekea katika uchaguzi mkuu mwaka 2025, hivyo kutokana na mafunzo haya watatakiwa kuyapeleka katika ngazi ya kata na matawi na kutuletea taarifa,”amefafanua