WADAU wa utalii kutoka nchi 38 duniani wamethibitisha kushiriki maonyesho ya kimataifa ya Karibu-Kili Fair yanayotarajiwa kuanza Juni 3 hadi 5 mwaka huu mkoani Arusha.
Akizungumza jijini Arusha, Mkurugenzi wa Kilifair Ltd ambao ndio waandaaji wa maonyesho hayo, Dominic Shoo,alisema lengo la maonyesho hayo kutangaza vivutio vilivyopo nchini.
Alisema mbali na nchi hizo akithibitisha ushiriki wao,pia waonyeshaji kwenye mabanda kutoka nchi 12 watashiriki.
“Mwaka huu tumepata urahisi wa kupata wageni mbalimbali duniani, sababu ya Royal Tour aliyofanya Rais Samia Suluhu Hassan imetusaidia kuitangaza nchi,hivyo Dunia inafahamu Tanzania,”alisema.
Alisema onyesho hilo litakuwa la kipekee, baada ya Dunia kukumbwa na janga la Covid-19 na kutakuwa na vivutio mbalimbali vilivyopo nchini.
“Katika maonyesho haya pia tunatarajia washiriki 380 kutoka nchi hizo na wengine kutoka nchi saba za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambao wametuomba tutangaze vivutio vilivyopo katika nchi hizo kama vivutio vya pamoja,”alisema.
Meneja wa Benki ya NMB, Kanda ya Kaskazini,Dismasi Prosper alisema wao pia ni miongoni mwa washiriki wa maonyesho hayo, wakiamini utalii ni sehemu kubwa ya uchumi Kanda ya Kaskazini.
Alisema pia katika kunyanyua sekta ya utalii pia wamefadhili Sh.milioni 59 katika maonyesho hayo ili yafane na kukidhi haja kwa wageni wafakaohudhuria katika kutangaza vivutio vilivyopo nchini.
“Sisi tumejipanga kuhudumia wageni wetu watakaokuja na waliopo kwa kutoa huduma bora ya kubadilisha fedha kwa kuweka mashine za ATM kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Kilimanjaro (KIA) na tumeboresha na kujenga mahusinao mazuri na wafanyabiashra mbalimbali wa sekta ya utalii,”alisema.
Mwisho