Na Moses Mashalla,
Baraza la madiwani la halmashauri ya jiji la Arusha limempitisha naibu meya wa jiji la Arusha,Veronica Hosea kwa kura 32 na kumfanya kutetea kiti chake kwa mara ya pili mfululizo.
Mbali na kumchagua kiongozi huyo pia baraza hilo limewachagua wenyeviti wa kamati mbalimbali za halmashauri hiyo ambapo Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)hakikuweka mgombea.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo msimamizi wa uchaguzi ambaye pia ni mstahiki meya wa jiji la Arusha,Maximillian Iranqe alisema madiwani walimpitisha Hosea kuwa naibu meya ambapo alijipatia kura 32 za ndiyo na hakuna kura iliyoharibika.
Hatahivyo,meya huyo alisema kwamba mara baada ya uchaguzi huo wamejipanga upya katika mwaka huu wa fedha 2022/23 katika kusimamia fedha za serikali na miradi mbalimbali ya maendeleo.
Alisema kwamba katika mwaka huu wa fedha jiji litakuwa makini kwa kuwa wana miradi mikubwa ya kimkakati ambayo ni ujenzi wa kituo kikuu cha mabasi na kituo kikubwa cha utalii katika mlima Suye.
“Jiji kwa sasa limepata taswira mpya hawa viongozi tuliowachagua wengi ni wajumbe wapya hivyo tutarajie hata mabadiliko makubwa katika kusimamia fedha na miradi ya maendeleo “alisema Meya Iranqe.
Hatahivyo,naibu meya mteule wa jiji la Arusha,Hosea alisema kwamba kilichomfanya arudi kutetea kiti chake ni ushirikiano na upendo baina yake na madiwani wenzake.
Amesema kuwa kazi yake atakayoanza nayo ni kuhamasisha wakinama jijini Arusha kuchangamkia mikopo inayotolewa na halmashauri hiyo ili kutoa fursa kwa kundi hilo ambalo linategemewa katika ngazi ya familia.
Hatahivyo,mbunge wa jimbo la Arusha Mjini,Mrisho Gambo aliwataka madiwani wote kutofanya mzaha na kuhakikisha wanaisimamia halmashauri hiyo kwa kukataa kuburuzwa kwenye vikao mbalimbali.
Gambo,akizungumza katika kikao hicho alisema kuwa pamoja na kwamba ofisi ya mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali kuendelea na kazi ya ukaguzi wa hesabu mbalimbali ndani ya halmashauri hiyo lakini hiyo haitoshi kuwafanya wao wasahau majukumu yao.
“Maoni yangu ni kwa madiwani kuwa serious (makini) na kukataa kuburuzwa kwenye vikao ni lazima muhakikishe mnaisimamia halmashauri kama wajibu wenu “alisema Gambo
Mwisho