Na Geofrey Stephen,ARUSHA
Warembo kutoka nchi nane duniani wametua nchini kwa lengo la kujionea vivutio mbalimbali hapa nchini na kutangaza utalii baada ya kuvutiwa na filamu ya Royal tour iliyochezwa na rais Samia Suluhu hasan .
Pamoja na mambo mengine warembo hao watatembelea na kujionea machimbo ya madini adimu duniani ya Tanzanite yanayopatikana katika mji mdogo wa Mererani,wilayani Simanjiro mkoa wa Manyara.
Akiongea na Vyombo vya habari kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Arusha, baada ya kuwapokea warembo hao,Mkuu wa Wilaya ya Monduli,Frank Mwaisumbe ,aliipongeza taasisi ya Miss Jungle international kwa kuwaleta warembo hao waweze kujionea vivutio mbalimbali hapa nchini na kuweza kuitangaza Tanzania kimataifa.
Amesema Tanzania inajivunia kuona Warembo hao kutoka mataifa mbalimbali Dunia wakija nchini hususani katika jiji la kitalii la Arusha tayari kwa kutembelea vivutio mbali mbali vinavyo patikana katika mkoa wa Arusha na vilivyoko nje ya Arusha
Amesema serikali imevutiwa kuwepo na shindano hilo la Jungle International kwani ni kuendelea kutangaza fursa za kibiashara na uwekezaji zilizopo nchini kwetu katika sekta mbalimbali.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa wilaya Mwaisumbe amesema Serikali ya awamu ya sita imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji na kuwaomba warembo hao kutoka nchi mbalimbali kuwa mabalozi wazuri kuiongelea nchi yetu baada ya ziara yao katika eneo la Machimbo ya Madini ya Tanzanite na vivutio vya utalii.
“Nawaomba mtakaporudi kwenu muwe mabalozi wa kutangaza kiswahili kutangaza utalii wa madini hasa Tanzanite inayopatikana Tanzania pekee pia msisahau kuhamasisha usafi na uhifadhi wa mazingira nchini na duniani kote”
Awali akitoa taarifa ya mashindano hayo Mratibu wa Mashindano hayo Meneja Uzalishaji na Miradi ,Martin Rajabu amesema kwamba mashindano ya Miss Jungle international yana washiriki 50 kutoka mataifa mbalimbali dunia.
“Ila kwa sasa washiriki waliofika hapa nchini wapo nane kutoka nchi za Europe Spain,Nigeria,Equatorial Guinea, Ghana,Kenya ,Zchekoslovakia,Turkey na Tanzania ikiwa ni sehemu ya maandslizi ya mashindano hayo”alisema
Amesema kwamba baada ya kutembelea machimbo ya Mererani watatembelea pia maeneo ya vivutio vya utalii na utamaduni sanjari na maeneo ya uwekezaji wa kibiashara kwa lengo la kutangaza utalii na uwekezaji wa biashara ikiwa ni sehemu moja wapo ya kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan kutangaza utalii wa ndani ambapo Rais Samia alipita katika migodi hiyo wakati wa kutangaza Royal Tour.
Baadhi ya warembo hao walisema wanajisikia vizuri kujionea uhalisia wa Tanzania baada ya kuona vivutio kupitia filamu ya Royal tour.
Ends…