*DKT. KIRUSWA ATOA MAAGIZO MAHSUSI MTWARA*
*Aitaka GST na STAMICO kufanya utafiti wa madini Lindi na Mtwara*
*Amuagiza Afisa Madini kutoa elimu ya usalama na utunzaji wa mazingira.
Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuwasadia wachimbaji wadogo wa madini katika mkoa wa Lindi na Mtwara kwa kuwafanyia tafiti za madini ili waweze kuchimba bila kubahatisha.
Dkt. Kiruswa ametoa agizo hilo baada ya kutembelea migodi ya wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu ya Utimbi na Upaso iliyopo katika wilaya ya Masasi mkoani Mtwara.
“Maeneo mengine katika mikoa ya Lindi na Mtwara hayajafanyiwa tafiti, hivyo nichukue fursa hii kuiagiza Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) pamoja na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kufika Lindi na Mtwara ili kuwasadia wachimbaji wadogo kufanyiwa tafiti kuliko kuchimba kwa kubahatisha,” amesema Dkt. Kiruswa.
Pia, Dkt. Kiruswa amemuagiza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mtwara Ephrahim Mushi kuhakikisha anatoa elimu ya usalama na utunzaji wa mazingira katika maeneo ya migodi mkoani humo.
Katika hatua nyingine, Dkt. Kiruswa ameelezwa changamoto zinazowakabili wachimbaji wa chumvi ambapo bei inayotolewa na mnunuzi wa chumvi ambaye ni mmoja Tanzania Nill salt ni ndogo ukilinganisha na gharama zinazotumika kuzalisha chumvi hiyo.
Sambamba na hayo Dkt. Kiruswa ametembelea mgodi wa madini ya Shaba uliopo katika kijiji cha Upaso ambao bado haujaanza uzalishaji na kumtaka Afisa Madini kutembelea mara kwa mara na kutoa elimu ya namna bora ya uchimbaji na utunzaji wa mazingira.
Pamoja na mambo mengine, Dkt. Kiruswa amewapongeza wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu kwa kuamua kufanya shughuli hiyo ambayo inaweza kuwabadilisha maisha yao na familia zao.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Lulindi Issa Mchungahela amempongeza Dkt. Kiruswa kwa kutembelea migodi ya madini katika wilaya ya Masasi ambapo amemuomba kuendelea kutoa elimu juu ya utunzaji wa mazingira.