Na WyEST,
ZANZIBAR
Wito umetolewa wa kufanya matayarisho ya kutosha ya matumizi ya lugha itakayokubalika kufundishia hasa kwa upande wa walimu na wanafunzi katika ngazi zote za Elimu nchini.
Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Mwanahamisi Ameir wakati akifungua kikaokazi cha maoni ya uchambuzi na tathmini ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 kinachofanyika Zanzibar.
Amesema kuwa matayarisho ya walimu upande wa mafunzo ni ya muhimu katika kuhakikisha walimu wapya wanaozalishwa na ambao wapo tayari kazini wanakuwa na vigezo vinavyotakiwa.
“Matayarisho ni ya muhimu kujua vitu kama sifa za wanaoenda kusomea ualimu, sifa za vyuo, muda wa mafunzo uweje, matayarisho ya walimu kumudu lugha husika ya kufundishia, vyote hivi vitolewe kwa kiwango katika vyuo vyote ili kupata walimu wenye sifa stahiki,” amefafanua Ameir.
Akiongea katika kikao hicho, Mwenyekiti wa timu ya Mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, Prof. Joseph Semboja amesema lengo la kikaokazi hicho ni kupokea maoni kutoka kwa wadau wa elimu kutoka upande wa Zanzibar juu ya maboresho ya Sera hiyo.
Kikaokazi hicho kinachotarajiwa kuhitimishwa kesho pia kimehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo, Jinsia, Wazee na Watoto, Abeda Rashid Abdallah na wadau mbalimbali wa Elimu kutoka Bara na Kisiwani humo.