Na Mwandishi wa A24Tv
Utata umeibuka kuhusu ujenzi wa jengo la biashara linalojengwa katika eneo la Ndovu jijini Arusha baada ya halmashauri ya jiji kuzuia ujenzi huo lakini mmiliki wake ambaye hajajulikana amekaidi na kuendelea na ujenzi kinyume cha sheria .
Ujenzi huo umeibua hali ya sintofahamu baada ya kujengwa katika mtindo wa maduka ya ndani(Kariakoo )kinyume na sheria za halmashauri ya jiji la Arusha zinazoelekeza majengo yote yanayojengwa katikati ya jiji yajengwe katika mtindo wa ghorofa.
Hatahivyo,taarifa za uhakika zinaeleza kuwa mmiliki wa jengo hilo anayetajwa ni kigogo wa Ccm Arusha (jina limehifadhiwa kwa sasa )anatumia nguvu na kivuli cha chama kuvunja sheria, jambo ambalo jamii inayozunguka jengo hilo imeziomba mamlaka za juu za chama hicho kikuu nchini kuingilia kati kwani anakichafua chama.
Baadhi ya wakazi wa Jiji la Arusha wamehoji kuhusu kitendo cha ujenzi huo kuendelea hadharani licha ya halmashauri ya jiji la Arusha kuweka alama ya X kuzuia ujenzi huo na kudai kwamba alama hiyo ingewekwa kwa raia wa kawaida bila shaka ijenzi ungesimama .
Wakazi wa mtaa wa Pangani walimtaja kigogo mzito wa Ccm wilayani Arusha kuwa ndiye mmiliki wa jengo hilo na amekuwa akionekana mara kwa mara katika eneo hilo huku wakidai kwa kuwa ni kiongozi wa Ccm hawezi kuguswa na mkono wa dola.
“Kwa kuwa ni kiongozi wa Ccm pamoja na jiji kuweka alama ya X kama ishara ya kuzuia ujenzi lakini huwezi kuona hatua zikichukuliwa sheria inachukuliwa kwa watu wasio na majina na fedha tu”alisema mfanyabiashara wa mchele katika eneo hilo ambaye hakupenda kutaja jina lake hadharani
Mkazi mwingine wa eneo hilo,Mohamed Abdul alisema kuwa aliwaona baadhi ya watumishi wa jiji la Arusha wakifika eneo la ujenzi na kuweka alama hizo na kisha kutokomea lakini cha ajabu anashangaa kuona ujenzi huo bado unaendelea.
Waandishi wa habari walifika katika eneo hilo kufuatilia taarifa hizo na walielekezwa kumuona msimamizi wa ujenzi aitwaye Akida ambaye hatahivyo juhudi za kumpata ziligonga mwamba baada ya kutoweka ghafla.
Hatahivyo,katika eneo la tukio mbali na kushuhudia maandishi yenye rangi nyekundi yaliyoandikwa “K/064 X kibali jiji” ” pia walishuhudia mafundi wakiwa wanajenga pasipokuzingatia kanuni za ujenzi kama kuvaa kofia ngumu na viatu maalumu vya ujenzi.
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya jiji la Arusha,Hargeney Chitukuro alipotafutwa na waandishi wa habari alisema kwamba hana taarifa hizo na kuomba apewe muda wa kuzifuatilia kabla ya kutoa taarifa rasmi.
“Sina taarifa hizo yaani wewe ndio unaniambia naomba unipe muda nifuatilie kwanza hizo taarifa alafu tuwasiliane”alisema Chitukuro.
Mwisho .