Moses Mashalla,
Waziri wa madini nchini,Dotto Biteko ametoa kauli kuhusu jiwe la madini ya Ruby lenye uzito wa kilo 2.8 lililoonekana Dubai kwenye maonyesho na kutamka kwamba serikali bado inachunguza
Waziri Biteko alitoa kauli hiyo hivi karibuni wakati akifungua mkutano wa tatu wa dharula wa baraza la mawaziri wa jumuiya ya nchi zinazozalisha almasi (ADPA) uliomalizika hivi karibuni jijini Arusha.
Akihojiwa na waandishi wa habari waziri Biteko alisema kwamba serikali bado inaendelea kuchunguza sakata hilo kwa kushirikisha vyombo mbalimbali serikalini.
“Bado tunaendelea na uchunguzi kwa kuwa tunashirikisha vyombo mbalimbali serikalini “alifafanua Biteko
Hatahivyo,alisisitiza kuwa hivi karibuni wizara itatoa majibu kuhusu jiwe hilo na kuwataka watanzania wawe na subira.
Hivi karibuni Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa alitoa ufafanuzi kuhusu Jiwe la Madini ya Ruby lenye uzito wa kilo 2.8 lililoonekana Dubai ambalo linasadikika kutoka Tanzania na kueleza kuwa, wizara inaendelea kufuatilia ukweli wa taarifa zake na endapo itapata nyaraka kuhusiana na jiwe hilo kama limetoka Tanzania, Taratibu na Sheria za Tanzania zitatumika katika kupata haki ya Tanzania.
Dkt Kiruswa alisema hayo katika bunge la bajeti lililomalizika hivi karibuni wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Mkinga Dunstan Kitandula ambaye alitaka kujua namna ambavyo Tanzania itanufaika na jiwe hilo.
Dkt. Kiruswa alifafanua kuwa, jiwe hilo linalosemekana kuwa na thamani ya Dola za Marekani milioni 120 ambazo ni sawa na zaidi ya shilingi bilioni 240 za kitanzania, taarifa zake zilionekana zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii ambapo wizara ilipata taarifa zake tarehe 13 Aprili, 2022.
Aliongeza kuwa, baada ya kupata taarifa hizo, wizara ilichukua hatua za haraka ili kujua kama habari hizo ni za kweli kwa kuanza kufanya ufuatiliaji kwa kuangalia taarifa za usafirishaji wa madini ya aina hiyo kwenye kanzidata zake na kubaini kutokuwepo kwa taarifa zinazofanana za jiwe hilo kwa uzito na thamani.
Akizungumzia mmliki halali wa jiwe hilo, amesema inasemekana huenda yupo nchini Marekani katika Jimbo la California na katika ufuatiliaji wa kupata chanzo halisi na asili ya jiwe hilo, nchi tatu (3) zinahusishwa ikiwemo Marekani, Umoja wa Falme za Kiarabu-Dubai na Tanzania.
Dkt. Kiruswa alisema kuwa wizara inawahakikishia watanzania kwamba itaendelea kusimama imara katika kudhibiti na kulinda rasilimali za watanzania kwa manufaa ya nchi hiyo.
Ilielezwa kuwa, jiwe hilo liliwekwa kwenye mnada wa mauzo ya madini baada ya mfungo wa mwezi Ramadhan kuisha ambapo lilitembezwa ili kuoneshwa katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dubai.
Mwisho.