Mkuu wa wilaya ya Arusha,Said Mtanda ameiamuru mamlaka ya usimamizi wa vyombo vya usafiri wa moto (Latra) mkoani Arusha kusitisha mara moja utoaji wa leseni za usafirishaji wa Bajaj mpaka pale serikali itakapojiridhisha mahitaji na idadi ya bajaji hizo jijini Arusha.
Pia amelielekeza jeshi la polisi mkoani Arusha kuwachukulia hatua kali za kisheria baadhi ya madereva bajaj jijini hapa ambao wamedaiwa kutumia silaha za mapanga,visu na nondo kuwashambulia madereva wa dalaladala hali ambayo imeibua mgogoro baina yao.
Mtanda ametoa kauli hiyo leo katika soko la Kilombero mara baada ya kufika hapo kutatua mgomo wa madereva wa daladala ambao walianzisha mgomo mapema leo asubuhi kufuatia madai ya kushindwa kufanya biashara baada ya kufanyiwa vurugu na madereva wa bajaji.
Akizungumza katika eneo hilo Mtanda alimuagiza afisa mfawidhi wa Latra mkoani Arusha,Aman Mwakalebela kusimamisha zoezi la usajili wa bajaji mpaka pale serikali itakapojiridhisha idadi ya bajaji na mahitaji yao katika wilaya ya Arusha.
“Ninakuelekeza Latra ninasimamisha zoezi la usajili wa bajaji mpaka pale nitakapojiridhisha idadi ya bajaji ziko ngapi na mahitaji yao” amesema Mtanda.
Hatahivyo,Mtanda amesisitiza kwamba serikali itafanya oparesheni maalumu kwa siku 14 kuanzia leo kufuatilia madereva wote wa bajaji wanaofanya kazi kinyume na kanuni walizoelekezwa.
Naye afisa mfawidhi wa Latra mkoani Arusha,Aman Mwakalebela amesema kwamba ofisi yake imepokea maelekezo hayo kwa kuwa tayari ilishasitisha usajili wa leseni kwa vyombo hivyo wiki moja iliyopita.
Mwakalebela amessma kwamba bajaji haziruhusiwi kufanya biashara ya kupakia na kushusha abiria kama daladala kwa mujibu wa sheria huku akisema kwa sasa zimesababisha kero kubwa jijini Arusha.
“Nilishasitisha kutoa leseni kwa bajaji wiki moja iliyopita na bajaji haziruhusiwi kufanya biashara kama daladala hii imekuwa kero sana ” amesema Mwakalebela
Hatahivyo,kiongozi wa maderava wa daladala jijini Arusha,Faraj Mrutu amewataka madereva wenzake kusitisha mgomo na kurejesha huduma kwa wananchi ili kusubiri maelekezo ya serikali baada ya siku saba.
Mrutu,amemuomba Mkuu wa wilaya ya Arusha kushughulikia suala la usalama kwa kuwa baadhi ya madereva daladala wamekuwa wakipigwa na madereva bajaji na kusisitiza hali ni mbaya kwa sasa endapo isipodhibitiwa.
Mwisho.