Na Geofrey Stephe Lushoto
Zaidi ya shilingi Bilioni 3.2 zimetumika katika Ujenzi wa jengo la Utawala la ghorofa mbili katika jimbo la Bumbuli Wilayani Lushoto Mkoani Tanga.
Jengo hilo ambalo litakuwa na vyumba 72 vya watumishi wa idara zote za Halmashauri ya Jimbo hilo linatarajiwa kukamilika ifikapo desemba mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa Habari wakati akitembelea miradi ya maendeleo katika Jimbo la Bumbulu,Mkuu wa Wilaya ya Lushoto,Kalist Lazaro alisema kuwa bajeti ya ujenzi wa ofisi za Halmashauri ni kiasi cha shilingi bilioni 4 na ujenzi umefika asilimia 90 mpaka kukamilika kwake.
Lazaro alisema kuwa Jimbo la Bumbuli lenye kilimo kikuu cha biashara ya Chai lilikuwa halina ofisi za uhakika za Halmashauri na ujenzi wa jengo la Utawala ni juhudi za Mbunge wa Jimbo hilo Januari Makamba ambaye ni Waziri wa Nishati.
Alisema kuwa anamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan jengo la Utawala la Halmashauri ya Bumbuli na ikiwezekana pia siku ya kuzinduliwa kwa jengo hilo mgeni rasmi awe Rais kwa hadhi ya jengo hilo.
‘’Hili jengo linapaswa kuzinduliwa na Rais kwa kuwa ni jengo lanye hadhi ya hali ya juu na limejengwa kisasa kuliko halmashauri yoyote katika ukanda wa kaskazini’’alisema Lazaro
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bumbuli,Magdalena Utouh alisema kuwa jengo hilo limefika hatua za mwisho kwani linatakiwa kukabidhiwa novemba 31 mwaka huu na fedha kwa ajili ya umaziaji ziko katika akaunti ya Halmashauri.
Alisema jengo hilo ambalo ujenzi unatekelezwa na SUMA JKT kwa stadi wa hali ya juu litakuwa jengo kubwa na la kisasa na wananchi wa jimbo hilo watakuwa wamezogezewa huduma karibu kwa ajili ya maendeleo ya jimbo lao.
Utouh aliendelea kusema kuwa zaidi ya shilingi milioni 150 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo na nyumba hiyo tayari imeshatumia zaidi ya shilingi milioni 48.5
Alisema kwa sasa ujenzi wa Nyumba hiyo uko katika hatua ya linta na ujenzi kwa sasa umesimama baada ya kukosekana fedha za kuendelea kwani walitarajia fedha kutoka katika vyanzo wa mapato vya Halmashauri hiyo.
Mkurugenzi alisema kuwa mbali ya ujenzi wa Nyumba ya Mkurugenzi pia zinahitajika nyumba zaidi kwa ajili ya wakuu wa idara pamoja na watumishi kwani nyumba za kupanga katika Halmashauri hiyo upatikanaji wake ni mgumu na zikipatikana baadhi hazina hadhi.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi{CCM} katika Wilaya ya Lushoto,Ally Daffa aliishukuru serikali kwa kuhakikisha jimbo la Bumbuli linakuwa na jengo lenye hadhi la Halmashauri na kuwataka watumishi wa Halmashuri hiyo kuhakikisha wanalitunza jengio hilo kwa masilahi yao wenyewe.
Alisema jengo walilokuwa wanatumia awali kama ofisi za Halmashauri halikuwa na hadhi lakini jengo lililojengwa kwa fedha za serikali shilingi bilioni 4 hadi kukamilika limeleta sifa katika jimbo hilo.
Mwenyekiti huyo alisema Rais ametimiza ahadi yake ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa wananchi wa Bumbuli kwa kuwajengea jengo la Utawala na miradi mingine ya maendeleo kwa ajili ya wananchi wa Jimbo hilo.
Mwisho