Na Mwandishi wa A24Tv Geita
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula akiwa ameambatana na Kamishna wa Tume ya Madini, Janet Lekashingo ametembelea banda la Wizara ya Madini, Tume ya Madini na Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) kwenye Maonesho ya Tano ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika Viwanja vya Bombambili, mjini Geita.
Katika Banda la Wizara ya Madini alielezwa kuhusu namna Wizara ya Madini inavyoandaa na kusimamia Sera na Sheria ya Madini pamoja na kanuni zake pamoja na mikakati iliyowekwa katika kuhakikisha watanzania wananufaika na Sekta ya Madini.
Katika banda la Tume ya Madini elimu ilitolewa katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na fursa za uwekezaji katika sekta ya madini, taratibu za upatikanaji wa leseni za madini nchini, biashara ya madini na taratibu za usalama wa afya na mazingira kwenye migodi ya madini.
Maeneo mengine ni pamoja na namna watanzania wanaweza kushiriki katika Sekta ya Madini kupitia utoaji wa huduma mbalimbali kwenye migodi ya madini na mchango wa kampuni za uchimbaji wa madini kwenye jamii.
Aidha Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) kilipata fursa ya kueleza majukumu na mikakati yake ya kuhakikisha elimu kuhusu uongezaji thamani inavyofanyika na kuongeza fursa za ajira nchini.