Na Mwandishi wa A24Tv.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara – Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah amesema Serikali imetoa vivutio vya uwekezaji katika Sekta ya Viwanda vya Dawa na Vifaa Tiba ikiwemo kupunguza Kodi ya Makampuni (corporate tax) kutoka 30% mpaka 20% kwa viwanda hivyo vipya kwa miaka mitano ya mwanzo ya uwekezaji sambamba na kutoa kodi kwenye vifungashio vya dawa.
Dkt Abdallah ameyasema hayo alipokuwa akizindua Kamati ya Kitaifa ya Kuratibu Masuala ya Viwanda vya Dawa na Vifaa Tiba na Warsha ya kutoa maoni kuhusu Rasimu ya Mkakati wa Kitaifa wa Kuendeleza Sekta ya Viwanda vya Dawa na Vifaa Tiba wa Mwaka 2022 iliyofanyika Oktoba 10, 2022 katika ukumbi wa JNICC Dar es Salaam.
Dkt. Abdallah pia amesema kuwa Serikali imeendelea kuweka na kusimamia Sera, Sheria na mikakati mbalimbali kwa lengo la kukuza na kuendeleza sekta hiyo changa ili kufikia malengo ya uwezo wa uzalishaji dawa nchini kwa asilimia 60 kutoka asilimia 12 ya sasa na kupunguza utegemezi wa kuagiza dawa hizo kutoka nje ya nchi.
Aidha, amesema Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara inaratibu shughuli za Uwekezaji, uzalishaji, na biashara wa sekta hiyo muhimu ili kufikia malengo yaliyoweka katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka 15 (Long-term Perspective Plan 2011/12 – 2025/26) na katika mipango mitatu ya miaka mitano ikijumuisha Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP II 2021/22 – 2025/26).
Dkt. Abdallah amewashauri washiriki wa warsha hiyo kutoa maoni yatayo wezesha kiwa na Mkakati Mkakati wa Kitaifa wa Maendeleo ya Sekta ya Dawa unao tekelezeka kwa kuweka mazingira bora na wezeshi ya uwekezaji, uzalishaji
na usambazaji wa dawa na vifaa tiba ili sekta hiyo ichangie katika ukuaji wa uchumi
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Viwanda wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Wilson Lugano akitoa maelezo mafupi amesema mchakato wa maandalizi ya Rasimu ya Mkakati huo umepitia awamu tatu zilizojumuisha utafiti sekta na ripoti uliofanywa na UNDP kwa kushirikiana na Wataalam Elekezi kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili wakiongozwa na Prof. Eliangiringa Kaale na Taasisi ya Usimamizi ya India kutoka Mji wa Calcutta.