Na Mwandishi wa A24Tv Singida
Mkuu wa wilaya ya Ikungi Mhe. Jerry C. Muro leo tarehe 09/12/2022 amewaongoza mamia ya wananchi katika Maazimisho ya sherehe za miaka 61 ya uhuru wa Tanzania Bara kwa kufanya kongamano la kihistoria lililowaleta wananchi, viongozi wa dini, wazee maarufu, watumishi wa umma na wafanyabiashara pamoja na wadau wa maendeleo wilaya ya Ikungi
Akitoa hotuba kwebye kongamano hilo Mhe. Muro amesema katika miaka 61 ya uhuru taifa limeweza kupambana na maadui watatu ambao ni ujinga, maradhi na umasikini kwa mafanikio makubwa kutokana na serikali za awamu zote kuwekeza vya kutosha katika mapambano ya kutokomeza maadui hao
Mhe. Muro amesema serikali ya awamu ya sita imewekeza vya kutosha katika sekta ya afya katika wilaya ya Ikungi ambapo zaidi ya bilioni 5 zimetolewa katika ujenzi wa hospital na vituo vya afya na zahanati pamoja na ununuzi wa dawa na vifaa tiba kwa lengo la kumtokomeza adui maradhi, vivyo hivyo kwenye sekta ya elimu ujenzi wa miundombinu ya madarasa, ukarabati wa shule kongwe, kuongeza walimu, kugharamia mpango wa elimu bure pamoja na kuongeza fedha za mikopo ya elimu ya juu na vyuo vikuu kwa lengo la kutokomeza adui ujinga ambapo katika wilaya ya ikungi zaidi ya Bilioni 3 zimetolewa katika awamu ya sita
Mhe. Muro amemaliza kwa kusema mfumo mpya wa uombaji na utoaji wa mikopo kupitia fedha za asilimia 10 zinazotengwa na halmashauri ya Ikungi pamoja na fedha za kusaidia kaya maskini kupitia TASAF zinalenga kutokomeza adui umaskini katika maeneo ya vijijini pamoja na mipango mingine ya kimkakati ya kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia fursa mbalimbali za uendelezaji biashara na mikopo nafuu katika taasisi za fedha.
Awali akizungumza katika kongamano hilo mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Ikungi Mheshimiwa Ali Juma Mwanga pamoja na mkurugenzi wa halmashauri hiyo Mheshimiwa Justice kijazi wamesema katika miaka 60 ijayo watahakikisha wanaweka misingi endelevu ya kuwakwamua wananchi kiuchumi mara baada ya kuimarisha mifumo ya utoaji wa huduma za jamii.
Kwa upande wao baadhi ya watoa mada kwenye kongamano hilo pamoja na kuelezea historia ya uhuru wa taifa la Tanzania wamesema taifa limefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kulinda na kutunza tunu ya amani umoja na mshikamano ambao umekuwa kichocheo cha maendeleo yaliyopo sasa
Akitoa salamu za chama cha mapinduzi wilaya ya Ikungi kaimu katibu wa wilaya Ndugu Shaban Muhimbani aliekiwakilisha chama cha mapinduzi katika kongamano hilo amesema katika miaka 61 ya uhuru chama cha mapinduzi kimeendelea kuonyesha taswira halisi ya maendeleo ya nchini kupitia ilani za awamu tofauti za chama cha mapinduzi na kusisitiza katika miaka mingine 60 ijayo chama cha mapinduzi kitahakikisha kasi ya maendeleo inaongezeka ili Tanzania iendane sambamba na nchi za dunia ya kwanza.
Mwisho