Na Mwandishi wetu, Mirerani
WATOTO 13 wakiwemo wasichana nane na wavulana watano wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, katika kuukaribisha mwaka mpya wa 2023 watachuana vikali kuwania ubingwa wa Mr & Miss Mazubu Grand Hotel.
Meneja wa Mazubu Grand Hotel, Charles Rioba amesema michuano hiyo kabambe inatarajiwa kufanyika leo Jumapili ya Januari mosi mwaka 2023 kwenye hoteli yao.
Meneja Rioba amesema watoto hao 13 watachuana kuwania nafasi hizo ambapo kwa wavulana mshindi wa kwanza atapata zawadi ya shilingi laki mbili na nusu, mshindi wa pili atapata zawadi ya shilingi laki moja na nusu na mshindi wa tatu atapata shilingi laki moja.
“Kwa upande wa wasichana nao mshindi wa kwanza atapata shilingi laki mbili na nusu, mshindi wa pili atapata shilingi laki moja na nusu mshindi wa tatu atajishindia shilingi 100,000” amesema Meneja Rioba.
Amesema pia kwenye maadhimisho ya kukaribisha mwaka mpya wa 2023 burudani mbalimbali zitapatikana Mazubu Grand Hotel ikiwemo muziki, michezo mbalimbali ya watoto, bwawa la kuogelea kwa kiingilio cha shilingi elfu tatu tuu.
“Tunawakaribisha watu wote kufika hotelini kwetu kwa wingi kuja kwenye sherehe ya mwaka mpya wa 2023 kwa kuangalia vipaji vya vijana wadogo wa Mirerani watakavyovionyesha wao binafsi,” amesema Meneja Rioba.
Hata hivyo, amesema mara baada ya mashindano hayo kumalizika hoteli hiyo imeandaa tafrija ndogo kwa wateja wao walioshirikiana nao kwa namna moja au nyingine kwa mwaka uliopita wa 2022
Baadhi ya washiriki wa mashindano hayo wamesema kwamba wamejiandaa ipasavyo kushiriki mashindano hayo na hatimaye kupata ushindi.
Washiriki hao wameeleza kuwa wamejiandaa kwenye kinyang’anyiro hicho ambapo wataonyesha vipaji vyao kwenye mavazi ya ubunifu, mavazi ya asili na mavazi la kutokea.
MWISHO