Na Doreen Aloyce, Dodoma
IMEELEZWA kuwa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa kazi kuhusu usajili wa sehemu za kazi pamoja na kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini imebainika uwepo wa ada ambazo zilikuwa zinaongeza gharama za uendeshaji na kuchangia sehemu nyingi za kazi kutokidhi matakwa ya Sheria na kufifisha ushindani wao kibiashara.
Aidha Osha ilipendekeza ada hizo kupunguzwa ama kufutwa ambapo Mhe. Rais wa Jamhuriya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan aliridhia ada hizo kufanyiwa marekebisho kwa kuondoa na kupunguza jumla ya Ada / Tozo kumi na tatu 13.
Hayo yamebainishwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa kazi Bi. Khadija Mwenda Jijini Dodoma wakati wa mkutano na waandishi wa habari alipokua akieleza utekelezaji wa majukumu ya Wakala pamoja na mafanikio Yaliyopatikana katika uongozi wa serikali ya awamu ya Sita.
Ada zilizoolewa ni pamoja na Ada ya Usajili wa eneo la kazi iliyokuwa ikitozwa kati ya Sh. 50,000 hadi Sh.1, 800,000, Ada ya fomu ya usajili sehemu za kazi iliyokuwa ikitozwa Sh. 2,000,Kufuta Faini zinazohusiana na ukosefu wa vifaa vya kuzimia moto ya Sh. 500,000, Kuondoa Ada ya Leseni ya Ithibati iliyokuwa inatozwa Sh 200,000 kwa mwaka, Ada ya Ushauri wa kitaalamu wa Usalama na Afya ya Sh 450,000”.Alisema Bi. Mwenda
wenda Ameendelea kusema Ada zingine Zilizofutwa kuwa ni Ada ya mafunzo ya elimu kwa umma iliyokuwa inatozwa kiasi cha Sh. 250,000 kwa kila mshiriki, Kupunguza ada ya uchunguzi wa ajali iliyokuwa ikitozwa Sh. 500,000 mpaka Sh. 120,000, Kuondoa ada ya Kipimo cha Mzio (Allergy test) iliyokuwa ikitozwa Sh. 25,000 kwa Mfanyakazi.
“Ndugu zangu Ada ya Kipimo cha Kilele cha Upumuaji (Peek Expiratory Flow test) iliyokuwa ikitozwa Sh. 10,000 kwa Mfanyakazi imefutwa , Tumepunguza ada ya huduma za ukaguzi wa mifumo ya umeme katika Vituo vya Mafuta vilivyopo vijijini kutoka Sh. 650,000 hadi Sh. 150,000. Punguzo hili lililenga kuhamasisha uwekezaji katika maeneo hayo, hivyo kupunguza athari zinazoweza kutokea kutokana na utunzaji wa mafuta kwenye chupa za maji na madumu, suala ambalo linahatarisha maisha ya wananchi katika maeneo hayo”Alisema
Amesema Mwakilishi wa Tanzania kutoka OSHA alishindanishwa na wataalamu 48 kutoka katika Nchi 16 za Jumuiya na hatimaye Mwakilishi huyo wa Tanzania, alifanikiwa kuchukua nafasi hiyo ambapo Pamoja na vigezo vingine vilivyotumika kupata mshindi, kigezo kimojawapo kilikuwa ni sifa ya Tanzania kuwa na mfumo madhubuti wa Usalama na Afya mahali pa kazi unaosimamia nguvu kazi na hatimaye kuwezesha kuwepo kwa ajira zenye staha.
“hatua hii ni mafanikio makubwa kwa nchi yetu na OSHA kwa kutambulika Kimataifa kwa kuwa na wataalam wenye uwezo wa kusimamia mifumo ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi kwa kuzingatia vigezo vya Kimataifa.”
Katika kusimamia Sheria ya Usalama na Afya kwa lengo la kuzuia ajali, magonjwa na vifo vitokanavyo na kazi, maeneo ya kazi ambayo hayakuzingatia Sheria na Kanuni za Usalama na Afya yalichukuliwa hatua mbali mbali za kisheria zikiwemo kupewa hati ya maboresho (Improvement Notice) ambapo maeneo ya kazi 1,588 yalipewa hati hizo na maeneo ya kazi mengine105 yalitozwa faini.
Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi ni Wakala wa serikali, chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu. Wakala huu ulianzishwa mnamo tarehe 31 Agosti, 2001 chini ya Sheria ya Wakala za Serikali Namba 30 ya mwaka 1997 kama sehemu ya maboresho katika utoaji wa Huduma za Serikali kwa Wananchi.
Kusudi la kuanzishwa kwa Wakala huu ilikuwa ni kupata chombo mahsusi cha Serikali chenye jukumu la kuboresha ustawi wa wafanyakazi kwa kusimamia Usalama na Afya mahali pa kazi kupitia Sheria Namba 5 ya Mwaka 2003.