Na Mwandishi wa A24tv .
Kaya zaidi ya 15 katika eneo la Tanganyika pekazi kata ya Moshono jijini Arusha, zimekumbwa na maji ya mvua yaliyojaa ndani ya nyumba zao kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha jijini hapa.
Wakiongea na waandishi wa habari waliotembelea eneo hilo,baadhi ya wananchi hao akiwemo balozi wa eneo hilo,Nicolas Kivuyo na Elisifa Zabron wamedai kwamba athari hiyo imekuja mara baada ya jeshi la wananchi kambi ya Tanganyika pekazi kuweka tuta na kuziba mkondo wa maji hali iliyosababisha maji hayo kuelekea kwenye makazi yao huku wakimtuhumu diwani wao Miriamu Kisawike kushindwa kuwasaidi huku akiwajibu majibu yasiyofaa.
Aidha wakazi hao wamedai kwamba adha hiyo imekuwa ikiwasumbua kwa muda mrefu huku wakimtupia lawama diwani wao ,Miriamu Kisawike kwa kushindwa kuwasaidia kukutana na uongozi wa jeshi na kujikuta wakiteseka na hivyo wameiomba serikali iwasidie kuondokana na adha hiyo.
Kwa upande wake mkuu wa kambi ya Jeshi hilo ya Tanganyija Pekasi,HAMIS KINGUYE alisema kuwa tuta waliloweka hawakuwa na nia ya kuzuia maji ila walifanya hivyo kwa lengo la marekebisho ya miundombinu ya barabara inayoingia katika kambi hiyo.
Hata hivyo alisisitiza kuwa hafahamu chochote kuhusu athari ya maji wanayopata wananchi ila aliwasihi kuboresha mitaro ya ili kuruhusu maji ya mvua kupita kirahisi na kuondoa athari inayowakumba kwa sasa.
Naye afisa mtendaji wa kata ya Moshono Anna Lebisa alisema anaufahamu vizuri mgogoro huo na alishawahi kwenda katika eneo hilo na kuwasihi wananchi kujenga tuta ili kuzuia maji kwenda kwenye makazi yao.
Jitihada za kumpata diwani wa kata ya Moshono, Miriamu Kisawike ili kuzungumzia madai ya wananchi hao hazikuweza kuzaa matunda kutokana na simu yake ya mkononi kuita muda mrefu bila kupokelewa.
Mwisho