Na Geofrey Stephen ,ARUSHA
Kanisa Katoliki jijini ARUSHA,limelaani vitendo vya ukatiki na ushoga vinavyozidi kushamiri kwa Kasi hapa nchini na kuwataka wazazi ,walezi na jamii kwa ujumla kukemea kwa nguvu zote ,vitendo hivyo vinavyochochewa na tamaduni za kigeni na kuathiri tamaduni za Kitanzania.
Rai hiyo imetolewa na paroko wa parokia ya moyo safi, jimbo kuu katoliki la Arusha,Padri ,Festus Mangwangi ,katika misa takatifu ya kufungisha ndoa 51 za waumini wa kanisa hilo,ikiwa ni mwitikio mkubwa kuwahi kutokea kwa wanandoa huku baadhi yao wakitoka madhehebu mengine na kujiunga na kanisa hilo.
Alisema vitendo vya ukatili ulawiti na ushoga kwa jamii ni majanga yanayolitia aibu taifa na yanapaswa kukemewa kwa nguvu zote kwa sababu yanaanzia kwenye familia kutokana na jamii kukosa upendo na malezi yasiozingatia maadili .
Alisema mwitikio wa wanandoa hao ni matokeo ya kampeni ya Kaya kwa Kaya ya kanisa hilo kuwaondoa waumini wake kwenye dhambi ya kuishi katika maisha ya uzinzi.
“Tukio hili la kushuhudia waumini 51 wakifunga ndoa leo limetokana na hamasa kubwa tulioifanya kila kaya wakati tunazungusha via shiria vya jubilei ya miaka 60 ya kanisa katoliki jimbo kuu katoliki la Arusha ,vikilenga kuwaimarisha waumini kiimani na kudumisha umoja ili jamii iishi kwa upendo”
Alisisitiza kuwa wale waliochagua kuishi mume na mke, wasiishi maisha ya kuzini bali waishi maisha ya ndoa na leo waumini 51 wameitikia wito wa kufunga ndoa na kuwataka wadumishe upendo katika maisha yao ili kupunguza matukio ya ukatili yanayotokana na mifarakano ya ndoa
Naye mwenyekiti wa parokia hiyo ,Fedelis Matolo alisema kampeni ya kanisa hilo kuelekea jubilee ya miaka 60 imezaa manufaa makubwa kwa waumini wa kanisa hilo kuhamasika kufunga ndoa.
“Hii sio mara ya kwanza kwa kanisa hili kufungisha ndoa nyingi ,mwaka jana waumini 49 walifunga ndoa huku wengi wao wakiwa ni wale waliokuwa wakiishi bila ndoa”
Aliwataka wanandoa kuzingatia malezi bora ya watoto wakiwa na wazazi wao hali itakayosaidia kuepusha mifarakano isiyo na tija.
Mmoja ya wanandoa hao, William Fedelis alisema kuwa maisha ya ndoa yanapunguza matukio ya ukatili miongoni mwa familia na kuwataka wazazi kujitenga na maisha ya uzinifu kwani yanaongeza ukatili kwa watoto mara baada ya wazazi kutengana.
Ends..