BRYSON MSHANA, TABORA
Mashindano ya umoja wa Michezo na taaluma kwa wanafunzi wa Shule za Mshingi Tanzania (UMITASHUMTA) yamefunguliwa Mjini Tabora ambapo yanafanyika kitaifa na kuhusisha mikoa yote ya Tanzania.
Mashindano hayo amabayo yanahusisha michezo mbalimbali yamefunguliwa Juni 03, 2023 na Naibu Katibu mkuu anayeshughulikia Elimu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI), Dr. Charles Msonde.
Katika hotuba yake Dr. Charles Msonde amesisitiza juu uadilifu wakati wa michezo ya UMITASHUMTA mwaka huu wa 2023, ikiwepo udhibiti wa wanamichezo wasioruhusiwa (MAMLUKI) ili kuipa heshima sekta ya michezo mashuleni.
Msonde amesisitiza juu kuzingatia miongozo iliyowekwa kwa ajilili ya kuendesha michezo hiyo, ili kuhakikisha kuwa malengo ya mashindano hayo yanafikiwa ikiwa ni kukuza michezo na sanaa katika shule na nchi kwa ujumla.
Kwa upande wake Mratibu wa michezo kutoka OR – TAMISEMI George Mbijima ambaye pia ni mwenyekiti wa mashindano hayo, amesema maandalizi yamekamililika na timu zote zimeshawasili Tabora kwa ajili ya mashindano.
“Mandalizi yote yamekamilika, tayari washiriki wote wameshawasili na wamefika salama wakiwa na ari ya kushindana tunaamini kuwa tutakuwa na mashindano bora kabisa mwaka huu” ameeleza Mbijima.
Akitoa maoni yake kuhusu michezo ya mwaka huu, Afisa Utamaduni Mwandamizi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Janeth Elias amewapongeza waandaji kwa maandalizi mazuri.
“Serikli kupitia waandaaji wamejitahidi sana kuboresha kila eneo, hii inaonyesha namna ambavyo vijana watayafurahia mashindano ya mwaka huu kwa kipindi chote watakachokuwa hapa Tabora, pongezi hizi ziende kwa Rais wetu Dk.Samia Suluhu Hassan” amesisitiza Bi. Janeth Elias.
Mashindano ya UMITASHUMTA & UMISETA mwaka 2023, yanaandaliwa na kusimamiwa na Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Mkoa wa Tabora ni mwenyeji wa mashindano haya kwa mwaka wa pili mfulululizo, ikiwa mwaka jana 2022 pia mashindano yaliandaliwa mkoani humo.
Mwisho.