Na Geofrey Stephen Arusha
WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) inatoa mafunzo ya siku tatu kwa wafanyabiashara wa mazao nje ya nchi ili waweze kurasimisha biashara zao.
Mafunzo hayo yanatolewa jijini Arusha kuanzia leo, Agosti 24 mpaka 26,2023 kwenye ukumbi wa hoteli ya GoldenRose.
Akifungua mafunzo hayo, Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Arusha, Ramadhani Madeleka amewataka wadanyabiashara kuchangamkia fursa hiyo ya kusajili makampuni na majina ya biashara zao ili zitambulike na wafanye kazi ya usafirishaji nje ya nchi bila vikwazo.
Amesema mafunzo hayo yanagharamiwa na serikali na elimu watakayoipata iwawezeshe kuwa tija kwenye shughuli zao baada ya kuelewa umuhimu wa kufanya biashara ndani ya mfumo rasmi.
“Mkifanya biashara zenu kwa mafanikio zitakuwa na faida kubwa kwenu na kwa Taifa ndiyo sababu serikali ikaamua kuleta mafunzo haya ikiamini ninyi ji wafanyabishara wazalendo na mnaojituma,” amesisitiza Madeleka.
Amesema kuwa mafunzo hayo yaliombwa na Wafanyabishara hao ili wapate uelewa wa usajili wa kampuni zao,kwa Waziri wa Viwanda na Biashara na serikali, Dk Ashatu Kijaji wakati alipofanya ziara mkoani Arusha.
Madeleka amewaomba wafanyabaishara hao kuhakikisha wanafuata taratibu zote za usajili na upataji leseni ili biashara zao zitambulike rasmi .
Kwa upande wake mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Isdor Nkindi, amesema mafunzo hayo wanayatoa kwa wafanyabaishara wanaouza mazao nje ya nchi ili waelewe umuhimu wa kurasimisha biashara zao na kupata leseni ili wafanye kazi kwa uhuru.
Amesema kuwa Serikali imesikiliza ombi la wafanyabiashara hao waliotska elimu ikawaagiza kutoa mafunzo hayo ili wakielewa waweze kufuata taratibu na kurasimisha biashara zao kwa kusajili kampuni au jina la biashara ili kupata leseni itakayowezesha kufanya baishara zao bila kikwazo.
Nkindi amesema Serikali imejenga mazingira rafiki kwa ajili ya kuwawezesha kufanya biashara zao bila kukwama.
“Hivi karibuni serikali ilitoa maelekezo kuwa haikatazi kufanya biashara ya kuuza mazao nje ya nchi isipokuwa wale wanaofanya hiyo biashara watekeleze sheria, taratibu, kanuni na miongozo iliyowekwa,” amesisitiza Nkini na kuongeza.
…Nawasihi mzingatie sheria kanuni na taratibu katika biashara zenu serikali ipo kuwawezesha na itaendelea kufanya hivyo,”.
Naye, Mfanyabiashara kutoka soko la Maasai, Agness Mushi amesema amesema mafunzo hayo yamemuwezesha kuelewa umuhimu wa kuboresha shughuli zake kwa kusajili kampuni.
Amesema kuwa awali alikuwa hajui namna ya kusajili kampuni huku akifanya biashara kwa hofu kwani alikuwa hana uhakika kama yuko sawa kisheria au la.
Naye Mao Chizma amesema kuwa ni vizuru kusajili biashara ikawa rasmi hivyo kuepuka kuindokana na usumbufu wa kufuatwa kuwa umevunja sheria.
“Kuvusha mazao nje ya nchi ilikuwa inatupa ugumu sana kwa sababu ulikuwa unaambiwa leta hiki au kile na haujui utavipatia wapi lakini kwa mafunzo haya tutapata leseni za kusafirishia nje itatusaidia sana,” amesema Chizma