Arusha Na Mwandishi wa A24Tv .
Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imewahukumu aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha Dk. John Marco Pima na wenzake wawili kifungo cha kwenda jela miaka ishirini baada ya kukutwa na hatia kwa makosa tisa ya uhujumu Uchumi ikiwemo la utakatishaji fedha.
Hukumu hiyo imetolewa leo Alhamisi Agosti 31, 2023 na Mhe. Hakimu Serafina Nsana kwa shauri namba 05/2023 la uhujumu uchumi, lililokuwa likiwakabili Dk. Pima na wenzake Bi Mariam Mshana aliyekuwa Mweka Hazina wa Halmashauri ya Jiji la Arusha na Bw. Innocent Gitubabu Maduhu, aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Mipango, Takwimu na Ufuatiliaji wa Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Washtakiwa wote watatu walifikishwa Mahakamani kujibu Makosa waliyotenda baada ya kushirikiana kuandaa nyaraka zilizopelekea hasara kwa Halmashauri ya Jiji la Arusha kiasi cha Shilingi Milioni Mia Moja na Tatu (Tshs. 103,000,000/=) ambapo fedha tajwa walizitumia kwa manufaa yao binafsi.
Mwisho .