Na Geofrey Stephen Simanjiro
Mashahidi wawili katika kesi inayowakabili wafanyakazi sita wa mgodi wa madini ya Tanzanite wa Gem & Rock Venture unamilikiwa na Mfanyabiashara Maarufu Jijini Arusha,Joel Mollel maarufu kwa jina la Saitoti wameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilayani Simanjiro jinsi walivyopigwa na hatimaye kupoteza fahamu.
Shahidi wa kwanza wa upande wa Jamhuri aliyejitambulisha kwa jina la Ezekiel Isack{30} mkaguzi wa migodi na baruti katika Wizara ya Madini alidai kuwa marchi 13 mwaka huu akiwa katika shughuli za ukaguzi katika mgodi wa saitoti ghafla alivamiwa na wafanyakazi wa Gem & Rock na kushambuliwa kwa vifaa vya uchimbaji na kujeruhiwa vibaya mwilini haswa mgongoni.
Isack ambaye alikuwa akiongozwa na Mwendesha Mashitaka wa Serikali,Grace Mgaya mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro,Charles Uiso alidai kuwa walikwenda kufanya ukaguzi baada ya Meneja wa Kampuni ya Franone inayochimba madini ya Tanzanite Kitalu C Mirerani kulalamika ofisi ya Wizara ya Madini kuwa Wafanyakazi wa Gem & Rock wamepiga baruti iliyosababisha moshi na vumbi na kuathili wafanyakazi wa Franone.
Alidai kuwa kabla ya kuanza ukaguzi ghafla yeye na wenzake wawili walivamiwa na wafanyakazi wa Gem & Rock na kupigwa kipigo kitakatifu kilichowapelekea kupata majeraha mazito na baadhi yao kukimbizwa hospital baada ya kupata fomu ya matibabu ya PF3 katika kituo cha Polisi Mirerani.
Akihojiwa na Wakili wa washitakiwa sita,Daudi Lairumbe shahidi huyo alidai kuwa walipokuwa wakifanya ukaguzi katika mgodi wa Gem & Rock hakukuwa na wafanyakazi wa kampuni hiyo na barua ya malalamiko ya kampuni ya Franone iliyoandikwa na Meneja Frank Mziwanda Kampuni ya Gem & Rock hawakupewa nakala ya malalamiko hayo.
Shahidi Isack alimjibu Wakili Lairumbe kuwa kanuni ya Wizara ya Madini zinaruhusu Mkaguzi wa Wizara kukagua bila ya kuwa na mtu yoyote kwani wanaruhusiwa pia kukagua bila ya kuwa na wafanyakazi wa walalamikiwa wala wanaolalamika.
Shahidi wa pili wa Jamhuri katika kesi hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Switbert Albogast{45} mfanyakazi wa Franone yeye alidai kuwa siku hiyo ya marchi 13 mwaka huu alijeruhiwa vibaya kichwani na mwilini na kutokwa damu nyingi na kisha kukimbizwa hospital kwa ajili ya matibabu na kabla ya kufika hospital alipewa PF3 kutoka kituo cha Polisi Mirerani.
Albogast alidai hayo wakati akiongozwa na Mwendesha Mashitaka Mgaya mbele ya Hakimu Uiso na kudai kuwa jeraha la kichwani na mwilini lilitokana na kipigo kutoka kwa wafanyakazi wa Gem & Rock na hatimaye kupoteza fahamu.
Alidai wafanyakazi wa Franone,Polisi,Usalama wa Taifa wote walitekwa na kuwekwa chini ya ulinzi na wafanyakazi wa Gem & Rock na baada ya kutekwa na kuwekwa chini ya ulinzi walipigwa na vifaa vya uchimbaji na baadhi yao walikuwa hoi kiafya na wengine walipoteza fahamu na kukimbizwa hospital.
Kesi hiyo imehairishwa hadi septemba 8 mwaka huu ambapo mashahidi wengine wanatarajiwa kutoa ushahidi katika mahakama hiyo kwani Hakimu Uiso alisema kuwa muda sio rafiki kwa kuwa alikuwa na kesi nyingine ambayo ni ya miaka mingi hivyo ilipaswa kumalizwa ndani ya wiki hiyo.
Wafanyakazi sita wanaokabiliwa na kesi hiyo ya shambulio na kujeruhu watumishi wa serikali ni pamoja na Petro Exsaud{48} mkazi wa Moshono Jijini Arusha,Mosses Kilelwa{45} Mkazi wa Mirerani Simanjiro,Daniel Siyaya{44} Mkazi wa Ilboru Arumeru Mkoani Arusha,Mosses Sirikwa{46} Mkazi wa Ilboru Arumeru,Dausen Mollel{58} Mkazi wa Ilboru Arumeru na Enock Nanyaro{32} Mkazi wa Moshono Jijini Arusha.
Wakati huo huo Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Simanjiro imertupilia mbali kesi ya kukaidi amri ya Wizara ya Madini iliyokuwa ikiwakabili washitakiwa wawili Joel Mollel maarufu kwa jina la Saitoti na Enock Nanyaro kwa maelezo kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kisheria kusikiliza kesi hiyo.
Mwisho