Na Mwandishi wa A24Tv TANGA –
Wazazi na Walezi wameaswa kujenga mahusuiano mazuri na walimu ili kumuwezesha mwanafunzi kuwa na uelewa mzuri,maadili mema na nidhamu iliyo bora.
Hayo yamebainishwa leo katika Mahafali ya Kuwaaga Wanafunzi wa darasa la Saba wa shule ya msingi Abdulfadhil Abbas Islamic iliyopo mkoani Tanga wanaotarajia kufanya mtihani wao wa kumaliza elimu ya Msingi mwezi septemba mwaka huu.
Akizungumza katika mahafali hayo mgeni rasmi ambaye ni mkurugenzi wa Taasisi ya Ahlul Bait East Afrika Syd Sheikh Sharif Alwi amesema katika elimu kuna nguzo mbili muhimu ambazo ni Wazazi na Walimu ambao wanapaswa kila mmoja kusimama nafasi yake vyema ili kumuwezesha mtoto kufikia malengo yanayotakikana.
Kwa upande wake meneja wa shule Sheikh Shafi Nina amewataka wazazi kuwalea watoto katika mazingira ya kuwa na hofu ya Mungu huku akitanabaisha kuwa matatizo makubwa katika elimu ni kukosekana ushirikiano baina ya walimu na wazazi.
Nae Mwalimu mkuu wa shule ya Msingi Abdulfadhil Abbas Islamic Leila Aboubakar amesema Shule imekuwa na ufaulu mzuri katika mitihani ya ushindani kwa mkoa na wilaya huku akiwataka wazazi kuwawezesha watoto kupata masomo ya ziada.
Shule ya Msingi Abdulfadhil Abbas Islamic mkoani Tanga ina jumla ya wanafunzi 289 huku wavulana wakiwa 154 na wasichana 136 na Mahafali haya ya mwaka 2023 ni ya Tatu tangu shule hiyo kuanzishwa yakienda sambamba na mahafali ya wanafunzi wanaomaliza chekechea na kutaraji kuanza msingi 2024.
Mwisho .