Na Mwandishi wetu, Arusha .
Arusha .Wanafunzi wa shule ya sekondari Oldadai iliyopo kata ya sokon 11 wilayani Arumeru mkoani Arusha wanatarajiwa kuondokana na adha ya maji iliyokuwa ikiwakabili muda mrefu baada ya kupata ufadhili wa ujenzi wa kisima cha maji kutoka shirika la Worldserve International Tanzania .
Aidha wanafunzi hao walikuwa wakitembea umbali mrefu na wakati mwingine kupitwa na vipindi vya masomo kwa ajili ya kufuata maji hayo ambayo hayakuwa salama kwa afya zao .
Mkuu wa shule hiyo, Loishiye Sironga aliyasema hayo mkoani Arusha wakati akizungumza katika mahafali ya 31 ya kidato cha nne shuleni hapo ambapo jumla ya wanafunzi 214 wamehitimu.
Amesema kuwa uwepo wa mradi huo wa maji kutoka kwa wafadhili hao utasaidia sana kupunguza adha waliyokuwa wakipata wanafunzi hao na kuweza kuokoa muda waliokuwa wakifuata maji kuweza kujisomea .
“Uwepo wa maji haya hapa shuleni utasaidia katika matumizi ya kupikia na kunywa,usafi wa madarasa na wanafunzi hasa wale wa hosteli, sambamba na kuendeleza kilimo cha mbogamboga na matunda shuleni hapo.”amesema .
Sironga amesema kuwa,shule hiyo imeendelea kupanda kitaaluma mwaka hadi mwaka na kushika nafasi za juu kiwilaya,ambapo ilifanikiwa kufuta daraja sifuri kwa miaka miwili mfululizo na kufuta daraja F katika baadhi ya masomo.
Aidha amesema kuwa, wanaishukuru serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwani katika kipindi cha miaka miwili (2021 na 2022 shule imepokea jumla ya shs 182,500,000 ambazo zimetumika katika kujenga miundombinu mbalimbali shuleni hapo .
Ametaja changamoto zinazowakabili kuwa ni pamoja na uchakavu wa miundombinu hasa madarasa,mwitikio mdogo wa wazazi kutoa chakula kwa watoto wao wawapo shuleni ,hivyo kupelekea baadhi ya wanafunzi kushindwa kumudu masomo ya mchana kwa sababu ya njaa ,upungufu wa matunda ya vyoo vya wanafunzi,ukosefu wa jengo la utawala na kutokuwa na uzio kuzunguka shule hiyo.
“Shule yetu ina mpango wa kuanzisha kidato cha tano na cha sita na kuongeza mabweni kwa ajili ya 0 level na A level huku malengo makubwa yakiwa ni kuongeza kiwango cha ufaulu shuleni hapo na kuweza kuwa shule ya kuigwa.”amesema Sironga.
Kwa upande wake mgenirasmi Mratibu wa mpango wa uwezeshaji shule kutoka shirika hilo ,Rebecca Mmbaga amesema kuwa, wamekuwa wakiwasaidia shule mbalimbali kuchimba visima vya maji na kuweza kuondokana na adha ya ukosefu wa maji safi na salama lengo likiwa ni kutoa elimu bora.
Mmbaga amesema kuwa, katika shule hiyo wameshaanza mchakato wa kuchimba kisima tayari na mradi huo.unatarajia kukamilika wiki ijayo ambapo utagharimu kiasi cha shs 90 milioni.
Nao baadhi ya wanafunzi wamesema kuwa , uwepo wa mradi huo wa maji shuleni hapo utaongeza kiwango cha ufaulu shuleni hapo kwani muda waliokuwa wakitumia kufuata maji umbali mrefu watautumia kwa ajili ya masomo .
Mwisho .