Na Geofrey Stephen Arusha .
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omar Kipanga amesema serikali imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika Taasisi za Elimu ya Juu nyanja ya tehama ili kusaidia kuzalisha wataalam wengi na mahiri watakaosaidia maendeleo ya uchumi wa kidigitali.
Mhe. Kipanga ametoa kauli hiyo leo Novemba 17, 2023 jijini Arusha wakati akifungua Maadhimisho ya Miaka 6 ya Kituo cha Umahiri katika TEHAMA Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM AIST), ambapo amesema ustawi wa baadaye wa uchumi wa Afrika utategemea kiwango cha uwekezaji katika sayansi, teknolojia na uvumbuzi.
‘’Suala la ubunifu litaendelea kuwa muhimu na kuwa kipaumbele katika ukuaji wa uchumi kupitia sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, usafirishaji, elimu na biashara. Katika miongo ijayo uwezo wa uvumbuzi ni muhimu kwa ajili ya ushindani kitaifa, kikanda na kimataifa’’ alisema Mhe. Kipanga
Aidha Mhe. Kipanga ameishukuru seriakali ya Ujerumani, kupitia Taasisi yake ya GIZ pamoja na DAAD kwa kufadhili mradi unaolenga kuwajengea uwezo wanafunzi wa eneo la Afrika Mashariki katika Masuala ya TEHAMA.
‘’Program hii inajikita zaidi kwenye masuala ya TEHAMA, na mnafahamu hivi sasa ulimwengu unapoelekea, tunasema dunia ipo kiganjani bila kuwafunza vijana wetu umahiri katika TEHAMA tutaendelea kubaki nyuma’’ alieleza Mhe. Kipanga.
Ameongeza kuwa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan imewajibika kikamilifu katika kufanya uwekezaji mkubwa kwanza kwenye miundombinu, kusomesha wataalam mbalimbali lakini pia katika kuhakikisha inaandaa bajeti ambayo itawezesha masuala ya tehama kutumika kwa ufanisi.
‘’Katika Mwaka wa fedha 2023/24 serikali imetenga zaidi ya Bilioni 9 kwa ajili ya kuwezesha bunifu mbalimbali Pamoja na Teknolojia zilizoibuliwa ili ziende kuwa bidhaa zitakazosaidia kutatua changamoto zinazokabili jamii yetu’’ alibainisha Mhe. Kipanga.
Nae Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia Prof. Maulilio Kipanyula amesema tangu kuanzishwa kwa Kituo hich cha Umahiri wameweza kuzalisha wahitimu 136 ambao wanatoka katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Prof. Kipanyula amesema kuwa kituo hicho kinajivunia mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kutoa ufadhili kwa Wanafunzi wote nchi za Afrika Mashariki kusoma katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela.
‘’Kama mnavyofahamu duniani kote tunazungumzia uchumi wa kidigitali, kazi yetu kubwa ni kuzalisha wanaafrika wenye uwezo wa teknolojia za kidigitali, ili kusukuma maendeleo ya kiuchumi na kuiwezesha Afrika Mashariki ishiriki kikamilifu katika uchumi wa kidigitali’’ alieleza Prof. Kipanyula.
Akizungumza kuhusu matarajio ya ufadhili kupitia Kituo cha Umahiri katika Tehama (NM-AIST) Mwakilishi wa Taasisi ya DAAD ya nchini Ujerumani Bettina Onyango amesema taasisi inajivunia kuona kituo hicho kimefanikiwa kuanzisha program za shahada za uzamili, na tayari kimezalisha wahitimu ambao ndio wanufaika kutoka nchi zote za Afrika Mashariki.”
Ameeleza kuwa serikali ya Ujerumani inalenga kuendeleza ushirikiano katika kukuza maendeleo ya wanataaluma katika Vyuo Vikuu ili kuongeza umahiri na kuchochea maendeleo katika sekta mbalimbali za uzalishaji.
Mwisho