Na Anangisye Mwateba-Arusha
Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeutaka Uongozi na watumishi wa Chuo cha Utalii Kampasi ya Arusha (NCT) kuwa wabunifu katika kuandika maandiko yanayoendana na hali halisi ya biashara ya utalii Duniani, kwani kutakapokuwa na maandiko ya kisasa yanayoshawishi uboreshaji wa biashara ya utalii ndivyo tutakavyo kuza biashara ya utalii na kuongeza mchango wa pato la taifa kutoka katika Chuo cha Utalii Tanzania
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula(Mb) alipokuwa akiongea na watumishi wa chuo hicho kilichopo maeneo ya Sakina Jijini Arusha
Mhe. Kitandula aliongeza kuwa ili chuo hicho kiwe hai na kuonekana lazima kuwepo na maandiko ya kibiashara yanayoshawishi wafadhili au serikali kutoa fedha kwa ajili ya maendeleo ya chuo.
Aidha, Mhe. Kitandula aliutaka uongozi wa chuo hicho kujipima au kujitathimini kwa kina namna ambavyo chuo hicho kitaweza kubeba mzigo mkubwa kutokana na mikakati ambayo imejiwekea na makubaliano waliyowekeana na taasisi mbalimbali ambazo chuo cha Utalii kitandaa wataalamu wa ukarimu wa taasisi hizo.
Sanjari na hayo, Mhe. kitandula amepongeza chuo hicho kwa jitihada na hatua mbalimbali wanazochukua katika kuhakikisha chuo kinatoa wahitimu walio bora na waliopata mafunzo kwa vitendo katika uhalisia wa biashara ya utalii inayoendela Duniani.
“Nawapongeza kwa ujenzi unaondelea katika eneo hili kwani kwa kufanya hivyo mtaongeza udahili wa wanafunzi katika fani mbalimbali zinazoendeshwa hapa chuoni” Alisema Mhe. Kitandula
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii kuzungumza, Mkuu wa Chuo cha Utalii Tanzania, Dkt. Florian Mtei ameushukuru uongozi wa wizara unaoongozwa Mhe. Angellah Kairuki Waziri wa Maliasili na Utalii kwa kuwa umekuwa karibu na Chuo katika kusaidia mambo mbalimbali kwa ajili ya ajili ya Maendeleo ya Chuo cha Utalii Tanzania
Mwisho .