Na John Mhala,Monduli
Mfanyabiashara Maarufu wa Madini ya Tanzanite Mkoani Arusha,Sanare Mollel maarufu kwa jina la Muller mkazi wa Kijiji cha Moita Bwawani kata ya Moita Bwawani wilayani Monduli Mkoani Arusha anatuhumiwa kuwapiga na kuwajeruhi wananchi na wafanyakazi wa idara ya ardhi Halmashauri ya Monduli na kuwatishia kwa silaha aina ya bastola kwa hatua yao ya kwenda katika Kijiji hicho na kupima ardhi ya eneo la malisho ekari 7000 kuwa eneo la makazi bila lidhaa ya wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari,Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi{CCM} Kata ya Moita Bwawani Loseriani Loibanguti Kimbele alisema kuwa Mulle aliamua kufanya hivyo na kikundi chake cha wahuni wakati ardhi hiyo yenye ukubwa huo imepitishwa katika vikao vyote vya Kitongoji , Kijiji hadi kata na kupata Baraka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Monduli,Happy Laizer na kuagiza watendaji wake wawili wa idara ya ardhi kuendelea na zoezi la upimaji kutoka eneo la malisho kuwa makazi.
Kimbele alisema yeye ndio mhanga mkubwa wa siku hiyo ya tukio kwani tukio lilitokea Desemba 4 mwaka huu majira ya saa 7 mchana na baada ya kuvurugu hizo alikwenda Polisi Monduli na alifungua jalada RB/971/2023 kuharibu mali na kutishiwa kuuawa kwa silaha na hadi sasa Mfanyabiashara huyo hajaitwa Polisi hadi sasa na anatamba kijiji hapo kuwa serikali yote wilayani Monduli ameiweka kiganjani na hataweza kufanywa chochote.
Alisema wakati akifanya vitendo vya kuwapiga wananchi na wafanyakazi wawili wa idara ya ardhi Monduli waliokuwa wakipima ardhi hiyo kwa kuweka alama za Bicon alikuwepo askari kata Inspekta Mathew na alimsihi tajiri huyo kuacha kufyatua risasi lakini jitihada hizo hazikuweza kuzaa matunda na kuamua alichofanya na kumwambia askari huyo kuwa yeye anajulikana kila kona ya nchi hii na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha,Justin Masejo hataweza kufanya chochote.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Moita Bwawana,Bruno Joseph Mollel yeye alisema kuwa hakuna kitu kimefanyika kwa kificho kwa kila kitu kilifanyika kwa uwazi na kuhudhuriwa na wananchi zaidi ya 500 wa kijiji hicho na kuidhinisha ardhi hiyo kutoa katika eneo la malisho na kuwa eneo la makazi na ndio maana eneo hilo serikali iliruhusu na kuwatuma wafanyakazi wawili idara ya ardhi kuipima ardhi hiyo na kila maazimio yapo Halmashuri na kwa Mkuu wa wilaya ya Monduli.
Mollel alisema uhuni uliofanywa na tajiri Muller na genge lake kutoka katika kijiji cha Kilimtindi wilayani Arumeru unapaswa kukomeshwa kwani mfanyabiashara huyo ana chuki,fitina na husuda kwa viongozi wa kijiji cha Moita Bwawani na viongozi wa kata wenye kuleta maendeleo ya kata hiyo kuliko yeye alivyofikiria.
Akijibu tuhuma hizo,Muller alikiri yenye na wenzake wenye kupinga utoaji ardhi waliungana kama kikundi na kwenda kuwazuia wafanyakazi wa idara ya ardhi kutoendelea kupima ardhi hiyo ya ekari 8000 na sio 7000 kuwa eneo la makazi badala ya malisho na pia alikiri kutoa bastola katika vurugu hizo lakini alifanya hivyo kwa ajili ya kujilinda kwani kundi la watu wenye silaha za jadi kama sime,mapanga ,mkuki na marungu lilikuwa likitaka kumvamia na kumzuri hivyo alivyatua risasi hewani na kuwatawanya na alifanikiwa kwa hilo.
Hata hivyo habari kutoka Polisi Monduli zinasema kuwa kweli bado Muller hajaitwa polisi kujibu tuhuma zinazomkabili kwa kuwa jalada hilo liko mikononi mwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Monduli{OC- CID] na alipotafutwa Kamanda wa polisi Mkoa wa Arusha kueleza ni kwani nini muda mwingi umepita bila mtuhumiwa kusakwa na kusamilisha silaha zake tatu simu yake ya kiganjaani ilikuwa haipatikani lakini juhudi za kumsaka bado zinaendele.
Mwisho