Doreen Aloyce, Dodoma
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara (Mb) Exaud Kigahe amesema Serikali kwa kushirikiana na Halmashauri zote nchini ipo tayari kuwasaidia wafanyabiashara na wajasiliamali katika nyanja mbalimbali ili waweze kutimiza ndoto zao za kiuwekezaji na kibiashara.
Mheshimiwa Kigahe ameyasema hayo ,Disemba Mosi Mwaka 2023 Jijini Dodoma wakati akifungua Kongamano la Biashara na Uwekezaji la Jiongeze lililoandaliwa na Wasafi Media.
Aidha amesema katika kutatua changamoto hiyo Serikali imeanzisha kitengo kamili kinachoshughulikia maswala ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara katika kila Halmashauri kote nchini.
Sanjari na hilo,amebainisha,kuwa Serikali imeanzisha Dirisha la Kielektroniki la Kuwahudumia Wawekezaji mahala pamoja (Tanzania Electronic Investment Window) ambalo ni mfumo wa Kidigitali ambao wawekezaji watautumia kujisajili na kupata vibali na leseni pamoja na kupata taarifa mbalimbali za uwekezaji.
“Kama mnavyojua kuwa nchi yetu katika maeneo mbalimbali imebarikiwa kuwa na fursa nyingi ambazo tunaweza kuzitumia ili kuinua uchumi wetu na wa nchi ikiwemo utalii, kilimo, ufugaji, uvuvi na madini niwasihi mchangamkie fursa hasa kwa hapa Dodoma ambapo ni makao makuu”amesema Mheshimiwa Kigahe……
” Serikali tunaunga mkono juhudi za Wasafi Media kuanzisha kongamano hili lililoenda sambamba na tamasha kubwa la muziki la Wasafi Festival na kupitia kongamano hili wadhubutu, kuanzisha biashara kufanya uwekezaji katika sekta na serikali tuwe tumepokea mawazo mbalimbali kuhusu namna ya kuboresha zaidi mazingira ya biashara na uwekezaji katika maeneo yetu”ameongeza Mheshimiwa Kigahe.
Katika hatua nyingine,Naibu Waziri huyo, amezitaka Taasisi zote zinazohusika na kuwasadia wafanyabiashara na wawekezaji hapa nchini kutimiza wajibu wao wa kuwahudumia wafanyabiashara kwa wakati na kuwawezesha kuwekeza, kuanzisha biashara katika maeneo yao jambo ambalo litasaidia kujiinua kiuchumi.
Licha ya hayo amewataka Wajasirianali hao kuwa na nidhamu katika kufanya biashara zao na kwamba serikali inataka kuhakikisha sekta binafsi inafikia uchumi wa kati.
Kwa upande wao wafanyabiashara walioshiriki kongamano hilo wamesema kuwa kupitia kongamano hilo ni fursa kwao katika kukuza biashara zao.
Mwisho.