Na Mwandishi wetu Dodoma na Halle- Ujerumani
Wizara ya Madini imepata fursa muhimu ya kutangaza Madini ya Lithium na Madini mengine Mkakati ambayo nchi imebarikiwa kuwa nayo katika Kongamano la LithiumDays23 linalofanyika kila mwaka mjini Halle nchini Ujerumani.
Katika kongamano hilo, Tanzania imepewa heshima ya kushiriki kwa njia ya mtandao na ana kwa ana ambapo Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Madini Augustine Olal kwa niaba ya Katibu Mkuu amewaongoza Wataalamu wa Wizara kushiriki kwa njia ya mtandao kutoka Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.
Aidha, katika kongamano hilo, Tanzania imepata nafasi muhimu ya kujitangaza kama nchi ijayo mshirika wa LithiumDays24 na mwandaaji mwenza wa kongamano hilo.
Akitoa wasilisho katika kongamano hilo, Olal amesema nchi ya Tanzania inao utajiri wa urithi wa kijiolojia unaofanana na nchi ya Congo DRC ambayo ni mzalishaji mkubwa wa madini muhimu na mkakati na kueleza kwamba, hiyo ni kiashiria tosha kuwa Tanzania inaweza kuwa mzalishaji mkubwa wa madini hayo ambayo kwa kiasi kikubwa bado hayajaguswa. Hivyo, uwekezaji unahitajika katika kutafiti na kuchimba madini hayo.
‘’Amana kubwa za madini ya lithium nchini Tanzania pamoja na akiba kubwa ya madini ya kobati na nikeli zinaiweka Tanzania kama mdau wa kimkakati katika mnyororo wa kimataifa wa mzalishaji wa madini kwa ajili ya magari ya kutumia umeme na suluhu ya nishati safi,’’ amesisitiza Olal.
Amewahakikishia kuwa, Serikali inayo dhamira ya dhati katika kukuza mazingira rafiki ya uwekezaji na inashiriki kikamilifu katika mageuzi ya Sera na maendeleo ya miundombinu ili kuwezesha uchimbaji wa madini hayo muhimu.
Pia, Olal ameongeza kuwa, kutokana na amani iliyopo nchini na usalama ni hakikisho tosha kwamba Tanzania ni sehemu salama ya kuwekeza katika Ukanda wa Afrika Mashariki na kusema inayo heshima kubwa kuwa sehemu ya kongamano hilo na inatazamia kuwa mshirika muhimu katika uendelezaji wa madini hayo.
Awali, akimkaribisha Kaimu Katibu Mkuu kutoa wasilisho katika kongamano hilo, mwandaaji mwenza wa kongamano hilo kutoka Taasisi ya Teknolojia na Uchumi wa Lithium, Halle nchini Ujerumani Prof. Dr. Gregor Borg ameielezea Tanzania kama mdau muhimu katika uzalishaji wa madini ya nishati safi na nchi iliyobarikiwa kwa utajiri wa madini mbalimbali.
Profesa Borg pia amewahi kushiriki katika shughuli nyingi za utafiti wa madini nchini Tanzania kwa kushirikiana na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST).
Kongamano la Lithium Days ni jukwaa linalotumika kubadilishana mawazo na maendeleo ya utafiti yanayohusu teknolojia ya lithium na madini mengine mkakati na matumizi yake.
Aidha, kongamano hilo huwaleta pamoja wataalam wa utafiti wa sekta ambao wanalenga kutafiti na kufanya ufumbuzi endelevu na ubunifu kuhusiana na hifadhi ya nishati ya umeme.
Vilevile, LithiumDays hutumika kama kitovu muhimu cha kuendeleza utafiti unaohusiana na litihium hatimaye kuchangia katika maendeleo ya vyanzo vya nishati safi na kusaidia juhudi za kimataifa na mabadiliko ya tabia nchi.
Tanzania inajiandaa kikamilifu kuhakikisha inakuwa miongoni mwa nchi wazalishaji wa madini ya lithium na mengine ya kimkakati kutokana na mahitaji makubwa ya madini hayo duniani katika siku za usoni .
Kwa upande wa Tanzania, kutokana na tafiti za awali zinaonesha uwepo wa madini ya Lithium kwa kiasi kikubwa katika Mkoa wa Dodoma.
Kampuni kadhaa ambazo zimeorodheshwa katika Soko la Hisa la nchini Australia zijulikanazo kama Liontonwn Resources Ltd (ASX: LTR) Cassius Mining Limited (ASX: CMD) Intra Energy Corporation Limited (ASX:IEC) na Auroch Minerals (ASX: AOU) zilizoonesha nia kutafiti madini ya lithium mkoani Dodoma, matokeo ya utafiti wake wa awali yalionesha matokeo chanya.
Mwisho .