Na mwandishi wetu Arusha.
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imewataka wafanyabiashara kuhakikisha kuwa wanasajili logo zao kabla ya kuanza kuzitumia ili kuepuka usumbufu wa kuibiwa logo na wafanyabiashara wengine na kisha kujikuta katika mgogoro wa kibiashara.
Afisa Usajili wa BRELA Bi. Julieth Kiwelu ameeleza hayo Desemba,1, 2023, Maafisa hao walipowatembelea baadhi ya wafanyabiashara wa jijini Arusha ili kujua changamoto wanazozipata wakati wa kupata huduma mbalimbali za Taasisi kwa lengo la kuzipatia ufumbuzi.
Wakiwa katika Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), Bi. Kiwelu amesema pamoja na kwamba huduma zote za BRELA zinatolewa kwa njia ya mtandao, bado kuna umuhimu wa kuwatembelea ili kujua wanakumbana na changamoto gani wakati wa kufanya maombi mbalimbali kwenye mfumo.
Bi. Kiwelu amesema baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakitumia logo kwenye bidhaa zao bila kuzisajili jambo ambalo husababisha migogoro ya kibiashara kutokana na ushindani uliopo sokoni baadhi yao huiga logo na kuzisajili kisha kuonekana ndiye mmiliki halali wa logo hiyo.
“Ninawashauri wafanyabiashara kuwa kabla haujaanza kufanya biashara hakikisha kwamba logo ya bidhaa yako inasajiliwa na BRELA ili ikiingia sokoni itashindana kihalali na atakayejaribu kuiga utakuwa na haki ya kumshitaki,” amefafanua Bi. Kiwelu.
Maafisa hao pia wametembelea kiwanda cha Magodoro cha Tanfoam Arusha, Kampuni inayosambaza viuatilifu ya Bajuta International na soko la ya Madini la Mkoa wa Arusha
Maafisa wa BRELA wako mkoani Arusha kwa muda wa wiki moja kutoa mafunzo kwa wafanyabiashara kuhusu masuala ya Miliki Ubunifu, ili kukuza uelewa juu ya umuhimu wa wafanyabiashara hao kusajili logo zao pamoja na vumbuzi mbalimbali ili waweza kunufaika nazo.
Wakiwa mkoani humo wametoa mafunzo kwa wafanyabiashara wa Arusha jiji pamoja na Halmashauri za wilaya ya Arusha, Meru na Longido.
Mwisho .