Na Mwandishi wa A24tv .
Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Elimu, Utamaduni na Michezo imeitaka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kuongeza kasi ya kuwezesha tafiti na bunifu zitakazo tatua changamoto zinazoikabili jamii na sekta mbalimbali.
Akizungumza Januari 20,2024 wakati wa ziara ya Kamati hiyo katika Ofisi za COSTECH Jijini Dar es Salaam Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Musa Siima amesema COSTECH ina wajibu wa kusimamia na kufanya tafiti mbalimbali zitakazoisaidia taifa katika kutatua changamoto mbalimbali pamoja na zile zitakazochagiza maendeleo.
Mhe. Siima amesema kuwa Kamati imefarijika kuwa Serikali kupitia Wizara inatoa fedha za Maendeleo kwa Tume ambazo zimewezesha kazi kubwa na nzuri kufanyika ambapo ameshauri kuongeza fedha ili zisaidie katika kuwezesha kuendeleza bunifu na kufanyika tafiti kwa haraka.
“Naipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwani katika bajeti yake tunaona namna ambavyo imetoa fedha za utafiti na maendeleo kwa COSTECH ambazo leo tumeshuhudia namna zilivyotumika vizuri” amesema Mwenyekiti huyo.
Aidha Mwenyekiti huyo ameipongeza Wizara kwa kuanzisha Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu almaarufu (MAKISATU) ambayo yameibua vijana na bunifu nyingi, huku akisisitiza Tume hiyo kuhakikisha wanabiasharisha bunifu zinazotokana na mashindano hayo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda akizungumza katika ziara hiyo amesema ili kuendelea kuchochea tafiti serikali pia imeanzisha Mashindano kwa wanasayansi wanaochapisha matokeo ya tafiti zao katika majarida ya Makubwa Kimataifa.
” tunatambua tafiti ni nyenzo inayochochea maendeleo, hivyo nawaomba Waheshimiwa tuwahimize wanasayansi wetu wachapishe kazi zao katika majarida ya Kimataifa ili kazi zao zitambilike na kutumika kimataifa,”amesema Prof. Mkenda
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dkt. Amos Nungu amewaambia Wabunge kuwa tume hiyo imefanya kazi mbalimbali ikiwemo kujenga maabara katika Kiwanda cha Uzalishaji wa Dawa Asilia na maabara ya kupima udogo katika Chuo Kikuu cha Sokoine pamoja na Miradi mingine ya Kimkakati katika Taasisi mbalimbali.
Mmoja wa wanufaika wa Miradi ya COSTECH Prof Gerald Misinzo amesema tume hiyo imemwezesha kupata kiasi cha shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya kufanya utafiti juu ya magonjwa ya mlipuko itakayosaidia nchi za Afrika kuwa na uwezo wa kukinga na kuzuia magonjwa hayo
“Nakushukuru Wizara ya Elimu,Sayansi naTeknolojia kupitia COSTECH imeniwezesha kupata Bilioni 2.5 kwa ajili ya utafiti wa magonjwa ya mlipuko ili kuwezesha kuwa na uwezo wa kujikinga na kuzuia magonjwa hayo kwa nchi za Afrika” amesema Prof. Gerald Mizinzo.
Mwisho .