Na Mwandishi wa A24tv.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Franklin Rwezimula amesema jumla ya Shule 96 za Sekondari teule zitaanza utekelezaji wa kutoa masomo ya Amali, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mitaala mipya ya elimu iliyoboreshwa.
Dkt. Rwezimula ametoa kauli hiyo Januari 08, 2024 mkoani Morogoro wakati akifungua mafunzo kwa walimu kutoka shule teule 28 za serikali na 68 zisizo za serikali ambazo zitaanza kutoa elimu ya sekondari mkondo wa Amali katika awamu ya kwanza.
Dkt. Rwezimula amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwani maono yake yameleta msukumo mkubwa na kupelekea kuwa na Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023.
Katibu Mkuu huyo amelipongeza Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) kwa kukamilisha kazi ya ukaguzi wa shule teule, Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kwa kuongoza maboresho ya Mitaala ya Elimu pamoja na VETA kwa kazi ya kusimamia maandalizi ya utekelezaji wa Mitaala ya Elimu ya Amali.³
Nae Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dkt. Aneth Komba amesema Elimu ya Sekondari Hatua ya Chini itaendelea kutolewa kwa muda wa miaka minne na imegawanyika katika mikondo miwili: Mkondo wa Elimu ya Jumla na Mkondo wa Elimu ya Amali.
“Mkondo wa Elimu ya Amali umegawanyika katika michepuo ya fani za Kilimo na ufugaji, Umakenika, Sanaa Bunifu, michezo, Ufugaji wa nyuki, Urembo, n.k. Pia Mwanafunzi atasoma masomo ya Hisabati, Elimu ya Biashara, Kingereza na Historia ya Tanzania na Maadili ili kupata stadi za msingi katika mawasiliano, stadi za maisha na uzalendo’’ alisema Dkt. Komba.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa NACTEVET Dkt. Adolf Rutayuga amesema mitaala inayotolewa imetengenezwa na VETA na kuhakikiwa na NACTVET, hivyo amezishukuru Taasisi hizo kwa kushiriki kikamilifu kukamilisha kazi hizo kwa ufanisi.
Mwisho.