Doreen Aloyce, Dodoma
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amewataka wananchi kuepuka matumizi yasiyo sahihi ya vidonge vya kuzuia mimba maarufu kama P2 ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza pale dawa hizo zinapotumika bila utaratibu ikiwemo mvurugiko wa hedhi.
Dkt. Mollel amesema hayo leo Jijini Dodoma kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu wakati akijibu swali Namba 163 ambapo swali hilo limeulizwa na Mbunge wa Viti Maalum, Dkt. Thea Medard Ntara aliyeuliza Je, kuna mpango gani wa kuruhusu Sayana Press kama njia ya Uzazi wa Mpango badala ya kutumia P2 bila utaratibu.
Amesema P2 ni njia ya dharura ya vidonge vya uzazi wa mpango ambayo hutumika kuzuia mimba kwa mwanamke aliyefanya tendo la kujamiiana bila kinga kwa mfano aliyebakwa au ametumia kondomu ikapasuka na anadhani anaweza kupata mimba asiyoitarajia wakati Sayana Press ni njia ya kuzuia kupata ujauzito kwa muda mrefu, hivyo matumizi ya kuzuia mimba kwa Sayana Press na P2 ni tofauti.
Hata hivyo Dkt. Mollel ameongeza kuwa Sayana Press imesajiliwa na TMDA na inapatikana kwenye vituo binafsi vya kutolea huduma za afya kwa wateja wanaohitaji.
Mwisho.