Na Richard Mrusha
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amefungua rasmi Maonesho ya kwanza ya asali kufanyika nchini Tanzania (Honey Show) huku akihamasisha Watanzania kujitokeza kuchangamkia fursa za ufugaji nyuki na uzalishaji wa asali ili kukuza vipato vyao.
Ameyasema hayo leo Juni 19,2024 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Amesema lengo la Maonesho hayo yenye kaulimbiu “Beyond Hives, Beyond Borders” ni kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa ufugaji nyuki, uongezaji thamani na uzalishaji wa asali.
Amesema sekta hiyo ndogo ya ufugaji nyuki ina nafasi kubwa katika uchumi, ajira, utunzaji wa mazingira, uhifadhi, tiba chakula ikizingatiwa kwamba kwa sasa inatoa ajira kwa si chini ya watu milioni mbili na mchango wake katika Uchumi na lishe kuwa mkubwa sana.
“Tumewakusanya hapa wafugaji nyuki na wazalishaji wa asali, walio kwenye mnyororo mzima wa utoaji wa huduma wanaotengeneza vifaa na wanaotoa elimu kwa wananchi ili waweze kunufaika na Sekta hii ndogo ya nyuki” amesema Mhe. Kairuki.
Amefafanua kuwa Maonesho hayo ni ya kipekee kwa sababu Tanzania inatarajia kuwa Mwenyeji wa Kongamano la 50 la Ufugaji Nyuki Duniani Septemba 2027, ambapo Tanzania itapokea si chini ya wafugaji nyuki takribani elfu kumi ambao wataambatana na wenza ,watoto, ndugu na marafiki.
Amesema kongamano hilo litasaidia kukuza Sekta ya nyuki sambamba na kuinufaisha sekta ya utalii kwa kuwa italeta watalii wengi zaidi kupitia tukio hilo ambalo pia litaonyesha namna gani Tanzania imepiga hatua katika ufugaji nyuki na asali.
“Kongamano hilo pia litawezesha kupata fursa za ufugaji nyuki na asali, kutengeneza soko, kwa wafugaji nyuki na wazalishaji wa asali, kuwepo kwa mafunzo ya namna bora ya kuweza kuzalisha, mizinga ya kisasa,matumizi ya teknolojia na ubunifu katika ufugaji nyuki na uzalishaji wa asali,upatikanaji wa mitaji kupitia taasisi zetu za fedha” amesema.
Waziri Kairuki ametumia fursa hiyo kuwakaribisha Watanzania wote kujitokeza kuchangamkia fursa za ufugaji nyuki na uzalishaji wa asali huku akisisitiza kuwa uwekezaji wake ni wa gharama nafuu lakini unazalisha faida kubwa.
“Watanzania ufugaji nyuki unalipa, mwezi wa saba Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inatarajia kusaini mkataba na nchi ya China kuwa mojawapo ya soko la asali na tunaamini soko litakuwa kubwa zaidi” amesema Mhe. Kairuki.
Awali katika hotuba yake amesema kuwa Tanzania ni nchi ya pili inayoongoza kwa uzalishaji wa asali Barani Afrika (baada ya Ethiopia) na msambazaji mkubwa wa asali kwa Umoja wa Ulaya kutoka Afrika huku ikikadiriwa kuwa na uwezo wa kuzalisha mazao ya nyuki takriban tani 138,000 za asali na tani 9,200 za nta kwa mwaka. Uzalishaji wa sasa unafikia takriban tani 32,691 za asali na tani 1,907 za nta.
“Tanzania inauza nje wastani wa tani 1,695 za asali na tani 467.5 za nta na inazalisha wastani wa mauzo ya dola za Marekani 10,730,294.12 kila mwaka”amesisitiza.
Naye, Rais wa Apimondia, Dkt. Jeff Pettis amesema kuwa ufugaji nyuki ni njia mojawapo ya kumtoa mtu katika umasikini huku akisisitiza kuwa nyuki ni rafiki wa mazingira na wana nguvu kwa kulinda mazingira asilia.
Aidha, amesema ni vyema kushirikiana kufanya kazi kwa pamoja kuuza bidhaa za asali katika masoko ya ndani na pia kufanyia kazi mnyororo mzima wa thamani wa mazao ya nyuki ili kuwapa walaji faraja kwamba wanapata asali halisi.
Katika hatua nyingine Dkt. Pettis ameridhishwa na asali ya Tanzania na kusema kuwa ina sifa nzuri kwenye Soko.
Maonesho hayo yamehudhuriwa na watu zaidi ya 500 kutoka nchini Tanzania pamoja na nchi za Zimbabwe, Kenya, Uganda, USA, UK, Spain, Lesotho, Botswana, South Africa, Egypt, Mauritius, China, Burundi, Turkey, Zambia na Pakistan.
Mwisho.