Na Geofrey Stephen Arusha .
WATAALAMU wa ununuzi na Ugavi hapa nchini wametakiwa kuwa wazalendo na kuzingatia maadili,weledi,kanuni na taratibu katika kutekeleza majukumu yao .
Hayo yamesemwa leo mkoani Arusha na Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha,Missaile Musa wakati akifungua mafunzo kwa wataalamu wa manunuzi yanayoendelea mjini hapa.
Mafunzo hayo ya siku mbili yameandaliwa na Bodi ya wataalamu wa ununuzi na ugavi(PSPTB)na kushirikisha wataalamu wa sekta hiyo toka halmashauri zote na sekretarieti ya mkoa wa Arusha.
Musa amewataka kujiepusha na vitendo vya rushwa na kujikita zaidi katika kusimamia kikamilifu fedha zote za umma zinazotengwa kwa ajili ya miradi mbalimbali.
“hakikisheni mnajifunza kwa umakini mkubwa kuandaa na kutunza mikataba,na mzingatie yaleyote mnayofunzishwa hapa ili mkitoka muende mkayatekeleze kwa vitedo”alisisitiza katibu Tawala huyo wa Mkoa.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya wataalamu wa ununuzi na ugavi hapa nchini(PSPTB)Godfred Mbanyi alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wataalamu hao juu ya sheria mpya ya ununuzi na namna ya kusimamia mikataba.
Alisema kuwa changamoto kubwa wanayokumbana nayo katika maeneo mengi hapa nchini ni wataalamu wa ununuzi kufanya kazi pasipo kusajiliwa na bodi hyo jambo ambalo ni kinyume cha sheria na kuwataka wale wote ambao hawajasajiliwa wajisajili mara moja.
“Natoa wito kuzingatia sheria kanuni na taratibu za manunuzi katika kutekeleza majukumu yenu,na nawataka wale wote ambao hawajasajiliwa na bodi kujisajili haraka iwezekanavyo kwani iko kwa mujibu wa sheria na anayefanya kazi bila kusajiliwa anavunja sheria za nchi”alisema Mbanyi.
Kwa upande wake mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo,Catherine Mwamasage ambaye ni Mkuu wa kitengo cha manunuzi kutoka TANAPA,aliipongeza PSPTB kwa kuwapatia mafunzo hayo na kusema kuwa yatawasaidia kupata maarifa zaidi na wataenda kuyafanyia kazi kwa vitendo.
Mwisho.