Na Mwandishi wa A24tv Arusha.
Jumla ya wateja 100 wamefanikiwa kushinda kitita cha Shilingi milioni 10 kutoka kwa benki ya NMB kupitia droo yake ya pili ya kampeni ya Mastabata la kibabe lililochezeshwa jana katika tawi la Clock tower jijini Arusha.
Washindi hao wamejinyakulia Kila mmoja Shilingi 100,000 katika Kampeni hii ya Mastabata la kibabe inayoendeshwa na benki ya NMB kwa wiki 12, kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya fedha kidigitali.
Akizungumza wakati wa kuzindua kampeni hiyo mikoa ya kanda ya Kaskazini, Meneja mwandamizi wa NMB kitengo cha kadi Manfredy Kayala amesema lengo ni kuunga mkono jitihada za serikali katika kuhamasisha wananchi kupunguza matumizi ya fedha taslimu.
“Kampeni hii ya miezi mitatu inahusisha wananchi wenye akaunti ya benki ya NMB ambao wanafanya manunuzi na malipo mbalimbali kwa kutumia kadi zao za benki hivyo wanaunganishwa moja kwa moja kwenye droo yetu inayowapatia washindi zawadi hizi zote zikiwa na thamani ya Shilingi milioni 300i.”amesema Kayala
Meneja wa Benki ya NMB kanda ya Kaskazini, Baraka Ladislaus amesema kuwa ziko faida nyingi za kufanya miamala kwa kutumia kadi ikiwemo usalama wa fedha dhidi ya wezi lakini pia zawadi mbalimbali wanazoshinda watumiaji wa huduma hizo.
Amesema kuwa malipo kwa kutumia kadi za NMB kwa sasa wamesambaza katika maeneo mbalimbali ya migahawa, vituo vya mafuta, madukani hadi supermarket kwa ndani hadi nje ya nchi.
“Tunajua msimu huu wa sikukuu tunaenda kuwa na matumizi makubwa ndio maana tunasisitiza huduma ya malipo ya kadi kuepuka kutapeliwa, kuibiwa au hata kupoteza fedha ukitembea nazo”.
Amesema kuwa wametenga zawadi ya shilingi milioni 300, kwa ajili ya kuwafikia washindi zaidi ya 2000 ambao kila wiki washindi 100 watapatikana na kujishindia shilingi 100,000.
Amesema kuwa droo hiyo itakayochezeshwa kwa wiki 12 itakuwa pia na washindi 15 wa kila mwezi watakaopatiwa shilingi 500,000 kila mmoja kwa miezi miwili, na wengine 10 watajishindia safari ya kwenda kutembelea mbuga za wanyama za Mikumi na Ngorongoro wakiwa na wenzi wao.
“lakini katika kuhitimisha Kampeni yetu tutachezesha Droo ya kupata washindi sita wa tiketi ya safari ya kwenda Dubai na mwenza wao kwa siku tano kufanya utalii na katika mji huo na gharama itagharamiwa na Benki ya NMB” amesema Baraka.
Uzinduzi wa Kampeni hiyo ilienda sambamba na droo ya papo kwa hapo na washindi 25 walipatikana waliozawadiwa, fedha taslimu shiligi 50,000 kila mmoja, kofia, miamvuli, chupa ya maji na wengine kulipiwa manunuzi ya bidhaa ndani ya supermarket hiyo yenye thamani ya shilingi 300,000.
Mmoja wa washindi hao Tumsifu Steven aliyeshinda kulipiwa bidhaa alisema kuwa amekuja katika eneo hilo kufanya manunuzi na kukutana na droo hiyo ambapo amefanikiwa kushinda kulipiwa manunuzi.
“Kiukweli nimefurahi sana kushinda droo hii maana imenipunguzia gharama za manunuzi kuelekea msimu huu wa sikukuu, lakini zaidi nimekuwa nikifaidika na zawadi mbalimbali kutoka kwenye benki ya NMB hata ninapofanya malipo kwa kutumia kadi narudishiwa kiasi cha fedha niichotumia, hakika nifurahia huduma hizi” amesema.
Mwisho.