Na Mosses Mashala Zanzibar
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza kuwa kuna ongezeko kubwa la Wawekezaji katika Sekta ya Utalii hatua inayochangia ukuaji wa Uchumi na Maendeleo ya nchi.
Amebainisha kuwa Ongezeko hilo la Wawekezaji pia linachangia Ongezeko la Watalii wanaotembelea nchini hali inayoiimarisha sekta ya Utalii.
Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo alipoweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Hoteli ya SSPD-BUHAIRAN iliyopo Bwejuu Mkoa Kusini Unguja Inayomilikiwa na Wawekezaji kutoka Falme za Kiarabu.
Aidha Rais Dk. Mwinyi amefahamisha Kuwa Faida za Utalii ni Kubwa kwa nchi katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kuwahimiza Wananchi kuendelea Kuwaunga Mkono Wawekezaji wanaowekeza maeneo mbalimbali.
Amezitaja faida hizo kuwa ni pamoja na fursa za Ajira kwa Vijana zile moja kwa moja na nyengine zisizo za moja kwa moja , Upatikanaji wa soķo kwa bidhaa zinazozalishwa na Wakulima na Wavuvi kwa bidhaa za Baharini na Ongezeko la Pato la Taifa.
Halikadhalika Rais Dk.Mwinyi amewapongeza Wananchi wa Bwejuu na Mkoa wa Kusini kwa Kuonesha Utayari wao na Kuwakaribisha Wawekezaji hao.
Wakati huohuo Rais Dk Mwinyi ameridhia Ombi lililowasilishwa na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Ayoub Muhammed Mahmoud kwa niaba ya Wananchi la kutengenezewa Barabara Ya Kilomita Tatu kwa Kiwango cha lami Kutoka Michamvi Mashariki hadi Michamvi Magharibi.
Ufunguzi wa Mradi huo ni miongoni mwa Shamrashamra za Sherehe za Miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mwisho